Ondoeni hofu Serikali inahakikisha mko salama kwa kutoa huduma bora za afya - Dkt. Mollel

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tulizo Shemu akimwelezea Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Godwin Mollel jinsi walivyomuhudumia mgonjwa aliyefanyiwa  upasuaji mdogo wa moyo wa bila kufungua kifua  wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi hiyo iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Godwin Mollel akiwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam


Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni msimamizi wa wodi ya watoto Theresa Marombe akimwelezea Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Godwin Mollel namna ambavyo wodi hiyo  inavyowahudumia watoto wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Godwin Mollel akimjulia hali mtoto Sophia Naminga anayetibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Dkt. Winnie Masakuya, na katikati ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Naiz Majani


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimwelezea Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Godwin Mollel namna ambavyo duka la dawa la Taasisi hiyo linavyohudumia wagonjwa  wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Godwin Mollel akizungumza na wagonjwa wanaosubiri kuingia katika vyumba vya madaktari katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Godwin Mollel akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mara baada ya kumalizika kwa ziara yake ya kikazi aliyoifanya leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Watano kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi

Na: JKCI

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amewataka wananchi kuondoa hofu kutokana na changamoto za kiafya wanazopitia bali waamini wako salama kwani Serikali iko kazini kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za afya na hivyo kuwa salama.

Mhe. Mollel ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wagonjwa wanaotibiwa kwenye Taasisi ya Moyo Jakaja Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuwashukuru wafanyakazi wa afya aliyoifanya leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Aliwasihi wagonjwa hao kufuata ushauri wa kitaalamu wanaopewa na madaktari wanaowatibu na unaotolewa na Wizara ya Afya kwa kufanya hivyo wataweza kuepukana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza na hivyo kuwa na afya njema.

“Ninawaomba wananchi muondoe hofu kwani ukiwa na hofu hata kinga za mwili zinashuka na hivyo kusababisha mwili kushindwa kukabiliana na magonjwa pale ambapo utavamiwa na vijidudu”,.

“Pale ambapo utakutana na changamoto mbalimbali za afya usisahau kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na  kumuomba Mungu akujalie afya njema kwani yeye ndiye kila kitu katika maisha yetu”, alisisitiza Dkt. Mollel.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Naibu Waziri kwa kuwatembelea na kupata muda wa kuzungumza na wagonjwa pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi hiyo.

Alisema mbali na Dunia kukabiliana na ugonjwa unaosababisha Virus vya Corona (COVID 19) kwa mwaka jana wa 2020Taasisi hiyo iliweza kutibu  wagonjwa 99,046 ambapo kati ya hao wagonjwa waliotibiwa na kurudi nyumbani (outpatient) walikuwa 94,079, waliolazwa (inpatients) walikuwa 3,306 waliofanyiwa upasuaji wa kutumia tundu dogo 1262 na upasuaji wa kufungua kifua wagonjwa 399.

 

Alisema Taasisi hiyo haina changamoto ya upatikanaji wa dawa na  vifaa tiba na kuongeza kuwa asilimia 52 ya mapato yao yanatokana na  dawa zinazotolewa kwa wagonjwa, maabara na vipimo vingine vya uchunguzi.

 

“Tunaishukuru Serikali kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na JKCI na kuhakikisha dawa zinapatikana katika Hospitali yetu na hii inasaidia wagonjwa kupata huduma zote za matibabu, vipimo na dawa bila ya usumbufu wowote”, alishukuru Prof. Janabi.

 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari