JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo jana jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo mara baada ya kuisaini jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akipokea zawadi ya Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kutoka na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore aliyefika katika taasisi hiyo jana pamoja na wataalamu wengine kwa ajili ya kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo. Zawadi hiyo imetoka kwa Rais wa Burkina Faso Mhe. Kapteni Ibrahimu Traore.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore, viongozi wa JKCI na wataalamu kutoka Burkina Faso mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
******************************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Burkina Faso wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi ya matibabu ya magonjwa ya moyo.
Hati
hizo zimesainiwa jana jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu
wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore.
Akizungumza
mara baada ya kusaini makubaliano hayo Dkt. Kisenge alisema makubaliano hayo yataimarisha
utoaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini
Burkina Faso na kuokoa maisha ya wananchi wenye matatizo ya moyo.
“Tumekubaliana
kuwasaidia katika kufanya tatifi, kuwafundisha wataalamu wa afya wakiwemo madaktari, wauguzi
na wataalamu wa vifaa tiba jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo na namna ya
kutumia vifaa tiba vya moyo pia watawatuma wagonjwa ambao wameshindwa
kuwafanyia upasuaji waje kutibiwa katika taasisi yetu”.
“Katika
kutoa mafunzo ya kuwatibu wagonjwa ya moyo kuna wataalamu wetu ambao watakwenda
Burkina Faso kufundisha na kuna wataalamu kutoka nchini humo watakaokuja kujifunza katika taasisi yetu”, alisema Dkt.
Kisenge.
Dkt.
Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kuhusiana na upatikanaji
wa vifaa tiba wamekubaliana wanunue katika Bohari ya Dawa (MSD) ambao ni wasambazaji wa
vifaa hivyo katika taasisi hiyo.
“Kwa
namna ya kipekee namshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuimarisha tiba ya magonjwa ya moyo katika taasisi yetu kitu ambacho kimesababisha nchi mbalimbali
kuja kujifunza namna ya kutoa matibabu
ya moyo katika nchi zao pia kuwaleta wagonjwa wao kutibiwa JKCI”.
“Pia
ninamshukuru Rais wa Bukina Faso Mhe. Kapteni Ibrahimu Traore kwa kuiamini nchi yetu na kuwatuma wataalamu
wake ambao tumesaini makubaliano nao ili nao kupitia sisi wawe taasisi bora ya
matibabu ya moyo na kufika hatua tuliyoifikia sisi na leo tumeingia katika
historia na Burkina Faso ya kutangaza utalii tiba ambao umekuja katika afya”,
alisema Dkt. Kisenge.
Kwa
upande wake Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya
wa Rais, Drissa Traore ambaye kwa mara
ya pili ameongoza timu hiyo ya wataalamu kuja hapa nchini alisema siku ya
kwanza walipotembelea JKCI walivutiwa kwa huduma wanazozitoa pamoja na uhusiano
mzuri wa uongozi wa manejimenti uliokuwepo baada ya kurudi nchini kwao walivichukuwa
hivyo vyote na kuvifanyia kazi.
“Ninawashukuru
maraisi wetu wa Burkina Faso Mhe. Kapteni Ibrahimu Traore na wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kuwa tayari kuimarisha huduma za afya katika nchi zao, nimevutiwa na JKCI
kwani haitoi huduma tu Tanzania bali Afrika nzima ndiyo maana nasi tumekuja kujifunza. Tunawategemea
sana katika mafunzo, tafiti na matibabu ya moyo kwa afya za watu wa Burkina Faso”,
alisema Traore.
Mapema mwezi wa pili mwaka huu
Rais wa Burkina Faso Mhe. Kapteni Ibrahimu Traore alituma timu ya wataalamu
kwenda kujifunza katika taasisi hiyo na kuona hatua walizopitia katika tiba ya moyo hadi
kuwa moja ya Taasisi zinazoongoza Barani Afrika kutoa huduma za kibingwa bobezi
ili nao waweze kujifunza na kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini humo.
Utiaji saini wa makubaliano hayo ni jitihada zilizofanywa na ubalozi wa Tanzania nchini Burkina Faso unaowakilisha nchi hiyo kutokea Abuja, Nigeria unaoongozwa na Mhe. Balozi Selestine Kakele ambao waliratibu mawasiliano ya JKCI na Burkina Faso na kuhakikisha yanafanyika na hatimaye kufanikisha kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya ushirikiano huo.
Comments
Post a Comment