JKCI na Shirika la UNA VOCE PER PADRE PIO la Italia wasaini mkataba wa kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo Afrika
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na
Rais wa Shirika la UNA VOCE PER PADRE PIO la nchini Italia Palumbo Vincenzo wakibadilishana
mkataba wa kuwatibu watoto wenye matatizo ya moyo barani Afrika wakati wa hafla fupi ya kusaini
mkataba huo iliyofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar
es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Rais wa Shirika la UNA VOCE PER PADRE PIO la nchini Italia Palumbo Vincenzo wakionesha mkataba wa kuwatibu watoto wenye matatizo ya moyo waliopo barani Afrika wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba huo iliyofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
*************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini mkataba wa kushirikiana na Shirika la UNA VOCE PER PADRE PIO lililopo nchini Italia kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo barani Africa.
Mkataba
huo umesainiwa leo jijini Dar es Saalam baada ya kuona maendeleo makubwa
yaliyopo katika Taasisi hiyo kwa ukubwa Afrika na Taasisi ya kipekee inayoweza
kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo barani Afrika.
Akizungumza
na waandishi wa habari wakati wa kusaini mkataba huo Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kupitia
mkataba huo Shirika la UNA VOCE PER PADRE PIO watakuwa wanawachukua watoto
wenye magonjwa ya moyo kutoka nchi mbalimbali Afrika na kuwafikisha JKCI kwa ajili
ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.
“Siku
ya jana Shirika hili limewaleta watoto watatu kutoka nchini Cameron ambao
tayari tumewapokea na watafanyiwa upasuaji wa moyo kesho”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt.
Kisenge alisema Shirika hilo limeingia mkataba na JKCI ili waweze kuchukua
watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo barani Afrika na kuwapeleka JKCI
kufanyiwa upasuaji wa moyo lakini pia kulipia gharama za matibabu ya watoto
hao.
“Kupitia
mkataba huu nchi yetu itaendelea kutangaza utalii tiba na hii ni kutokana na
uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia Rais wetu Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwenye vifaa tiba na rasilimali watu”, alisema Dkt.
Kisenge.
Kwa upande wake Rais wa Shirika la UNA VOCE
RER PADRE PIO la nchini Italia Palumbo Vincenzo alisema Shirika hilo
linathamini maisha ya watoto hivyo kuona umuhimu wa kuwasaidia kwa njia
mbalimbali ikiwemo kusaini mkataba na JKCI kwani wakiokoa maisha hata ya mtoto
mmoja ni muhimu kwao.
Vincenzo alisema wamekuwa wakiifahamu JKCI
kuwa ni taasisi kubwa na yenye viwango vya juu katika kutoa huduma za upasuaji
wa moyo barani Afrika na kutokana na uhaba wa huduma hizi katika nchi nyingine
za Afrika wakaona ni vizuri kuitumia JKCI kuokoa maisha ya watoto.
Vincenzo alisema wanaona fahari na bahati
kubwa kushirikiana na kusaini makubaliano na JKCI kwani ni Taasisi kubwa yenye
viwango vya juu Afrika hivyo kuifanya Tanzania kuwa kituo kikubwa cha matibabu
ya magonjwa ya moyo Afrika.
“Tunawashukuru kwa kutupa nafasi hii
kushirikiana nanyi, tunaahidi kuwa sehemu ya kuleta maendeleao katika kutoa
huduma za upasuaji wa moyo na tutaitangaza Tanzania kama kituo kikubwa cha
kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto”, alisema Vincenzo.
Naye
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Angela Muhozya alisema Shirika hilo kutoka Italia limekubali kufanya kazi na
JKCI ya kuwasaidia watoto wa Afrika wanaohitaji kupata huduma ya matibabu ya
moyo.
JKCI
imekuwa ikifanya matibabu ya upasuaji wa moyo kwa kiwango kikubwa lakini katika
Africa ndio Taasisi pekee inayofanya upasuaji wa aina mbalimbali na ule
ambao ni mgumu kwa watoto wenye magonjwa
ya moyo.
“Tunashukuru tumepata washirika ambao wataweza kusaidia kuwalipia na kuwawezesha watoto kutoka nchi za Afrika kupata matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa moyo ambayo hawawezi kuyapata katika nchi zao”, alisema Dkt. Angela.
Comments
Post a Comment