Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma
Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi tuzo ya
shukrani kutokana na mchango wake alioutoa katika taasisi hiyo aliyekuwa Mkuu
wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi JKCI Dar Group Iddi Lemmah ambaye amestaafu kwa
mujibu wa sheria wakati wa hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika jana katika
ukumbi wa Taasisi ya hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi
wa Utawala na Rasiliamali Watu wa JKCI
Ghati Chacha.
Mkurugenzi wa Utawala
na Rasiliamali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha
akimkabidhi cheti cha shukrani kutokana na mchango wake wa utendaji kazi
alioutoa katika taasisi hiyo aliyekuwa
Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi JKCI Dar Group Iddi Lemmah wakati
wa hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika jana katika ukumbi wa Taasisi ya hiyo
iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha
Ununuzi na Ugavi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group Iddi Lemmah
akikata kike wakati wa hafla fupi ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake
katika utumishi wa umma iliyofanyika jana katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge na kulia ni Mkurugenzi wa JKCI Dar
Group Dkt. Tulizo Shem.
Aliyekuwa Mkuu wa
Kitengo cha Ununuzi na Ugavi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group Iddi Lemmah akitoa neno la shukrani
wakati wa hafla fupi ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi wa umma iliyofanyika jana katika
ukumbi wa taasisi hiyo iliyopo jijini
Dar es Salaam.
Na JKCI
*********************************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia nidhamu ya kazi ili waweze kustaafu kwa heshima katika utumishi wa umma.
Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge, wakati wa hafla fupi ya kumuaga Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa JKCI Dar Group, Iddi Lemmah, aliyefikia ukomo wa utumishi wa umma.
Dkt. Kisenge, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, alisema nidhamu ya kazi ni nguzo muhimu ya maendeleo, hususan katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kukwamisha juhudi za mabadiliko.
“Leo tunamuaga mtumishi mwenzetu ambaye ametoa mchango mkubwa kwa Taasisi, hususan katika eneo la ununuzi na ugavi. Amefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi milioni 500 na kutekeleza kwa ufanisi majukumu yenye kuhitaji ubunifu, fikra pevu na utaalamu wa hali ya juu,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake, Mkuu huyo wa Ununuzi na Ugavi wa JKCI Dar Group, Iddi Lemmah, alisema ubunifu na ujuzi alioutumia katika kipindi chote cha utumishi wake umechangia kuleta mabadiliko yenye tija kwa taifa.
“Nilianza kazi nikiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 22 na sasa ninastaafu. Katika kipindi chote cha utumishi wangu, nimezingatia nidhamu ya hali ya juu, nikiongozwa na kauli ya Hayati Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere, kwamba fedha siyo msingi wa maendeleo bali bidii ya kazi ndiyo msingi wake,” alisema Lemmah.
Naye Mkurugenzi wa JKCI Dar Group, Dkt. Tulizo Shemu, alisema mtumishi huyo amekuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na kujituma bila kuchoka.
“Amekuwa mstari wa mbele katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya ununuzi na ugavi ndani ya Taasisi, akihakikisha kazi zinafanyika kwa haraka, kwa ubora na kwa kuokoa muda. Aidha, alishiriki kikamilifu katika kamati mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya JKCI Dar Group,” alisema Dkt. Shemu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi wa JKCI, Robert Mallya, alisema amefanya kazi kwa karibu na Lemmah na kumtaja kuwa mtumishi mahiri aliyekuwa kiungo muhimu katika maendeleo ya Taasisi.
“Alikuwa mtumishi mwenye ushirikiano mkubwa, uzoefu wa
hali ya juu na ari ya kujituma, akitumia utaalamu wake kurahisisha utekelezaji
wa majukumu ya umma,” alisema Mallya.






Comments
Post a Comment