Madaktari waonya: Usisubiri dalili za Moyo zionekane ndipo uanze uchunguzi
Daktari bingwa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Theophilly Mushi akitoa elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa
ya moyo kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA)
wakati wa kambi maalumu ya elimu na uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa
LATRA iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Afisa Muuguzi mbobezi wa
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Happiness Muragwa akimpima kiwango cha
sukari kwenye damu Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini
(LATRA) Rukia Kibwana wakati wa kambi maalumu ya kutoa elimu na uchunguzi
wa afya kwa wafanyakazi wa LATRA iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Edward Martin akitoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa Kaimu
Meneja Leseni za Usafiri wa Barabara wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini
(LATRA) Pateli Ngereza wakati wa kambi maalumu ya kutoa elimu na uchunguzi
wa afya kwa wafanyakazi wa LATRA iliyofanyika jana katika ofisi za LATRA jijini Dar es Salaam.
Na JKCI
********************************************************************************************************
Wafanyakazi nchini wamehimizwa kujenga
utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kujua namba zao za afya na
kutambua mapema viashiria muhimu vya mwili vinavyoweza kusababisha magonjwa ya
moyo, shinikizo la damu na magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Wito huo umetolewa na Daktari Bingwa
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theophilly Mushi wakati akitoa mafunzo
kwenye kambi ya upimaji wa afya kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri
Ardhini (LATRA) jijini Dar es Salaam.
Kambi hiyo ya upimaji na utoaji wa
elimu ililenga kuongeza uelewa wa wafanyakazi hao kuhusu magonjwa ya moyo na
magonjwa mengine yasiyoambukiza pamoja na namna ya kujikinga ili kuimarisha
afya zao na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Akitoa elimu kuhusu magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo Dkt. Theophilly alisema watu wengi hupata
matatizo ya moyo bila kutambua dalili au chanzo chake mapema.
“Unaweza kujikuta unapata maumivu ya
kifua kutokana na mbano wa mishipa inayosafirisha damu kwenda kwenye moyo kwa
sababu ya mafuta mengi mwilini hali inayoweza
kusababisha ugonjwa wa mishipa ya damu ya moyo kuziba”, alisema Dkt.
Theophilly.
Alifafanua kuwa kuziba kwa mishipa ya
damu ya moyo kunatokana na mafuta mengi mwilini pia ni moja ya sababu kubwa ya
maumivu ya kifua na matatizo ya moyo.
Dkt. Theophilly alisema baadhi ya
wagonjwa wa moyo hupata changamoto ya mfumo wa umeme wa moyo ambapo mapigo ya
moyo hupungua na wakati mwingine hulazimika kuwekewa kifaa maalumu cha kusaidia
moyo kufanya kazi.
“Usisubiri hadi uanze kuona dalili
kama kuvimba miguu, kushindwa kutembea au kupooza upande mmoja wa mwili kwani
wakati huo madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi”, aliongeza.
Dkt. Theophilly alisisitiza umuhimu wa
uchunguzi wa mapema wa afya ya moyo na kuchukua tahadhari kabla ya ugonjwa
kufikia hatua ya hatari.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa
LATRA Mambwana Jumbe alisema wataalamu wa JKCI wamekuwa na mchango mkubwa kwa
kutoa elimu ya afya kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo.
“Wataalamu wa JKCI wamekuja hapa LATRA
na kutupatia elimu muhimu kuhusu namna ya kulinda afya ya moyo na kujikinga na
magonjwa yasiyoambukiza. Elimu hii ni muhimu kwa watumishi wetu”, alisema
Mambwana.
Naye Afisa Leseni na Usajili wa LATRA,
Denis Daudi alisema mafunzo hayo yamewasaidia wafanyazi hao kuelewa namna ya
kujikinga na magonjwa yanayoathiri utendaji kazi wa mwili.
“Tumepata elimu ya kujikinga na
magonjwa yanayotokana na mtindo mbaya wa
maisha na yale yasiyoambukiza yanayoathiri afya na utendaji kazi. Elimu hii
itatusaidia kuchukua tahadhari mapema”, alisema Denis.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu
kujikinga na magonjwa yasiyoambukiz hususan ya moyo ili kupunguza athari zake
katika jamii na maeneo ya kazi.
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment