Matumizi ya shisha na sigara kusababisha magonjwa ya moyo, matatizo ya mapafu na saratani


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuzindua taarifa ya mwaka 2025 kuhusu  Kampuni za Tumbaku zinavyoingilia Sera ya Afya nchini iliyofanywa na Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF) katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.


Na JKCI
*************************************************************************************************

Vijana na wananchi kwa ujumla wametakiwa kutunza afya zao na kujiepusha na matumizi ya tumbaku hususani sigara na shisha yanayoweza kupelekea magonjwa ya moyo, matatizo ya mapafu na saratani hivyo kusababisha vifo vya ghafla.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge hivi karibuni wakati wa hafla fupi ya kuzindua taarifa ya mwaka 2025 kuhusu  Kampuni za Tumbaku zinavyoingilia Sera ya Afya nchini iliyofanywa na Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF) katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa wa moyo alisema matumizi ya tumbaku yanachangia kwa kiasi kikubwa kusababisha vifo vya gafla vinasababishwa na madhara ya tumbaku katika mishipa ya moyo ya damu inayopelekea magonjwa ya moyo.

“Matumizi ya tumbaku kwa vijana hususani katika nchi za Afrika Mashariki yanaongezeka kwa kasi ikiwemo uvutaji wa kisasa wa sigara aina ya shisha kwani kuvuta shisha mara moja ni sawa na kuvuta sigara 100 jambo ambalo lina madhara makubwa kwenye mishipa ya damu ya moyo inayoweza kusababisha mgando wa damu kwenye misuli ya moyo na kusababisha vifo vya ghafla”,

“Sigara pia inaweza kuleta madhara kwenye mapafu, kusababisha magonjwa ya saratani na kusababisha tatizo la kiharusi hivyo wananchi hususani vijana wanatakiwa kuchukua tahadhari mapema ili kujiepusha na madhara ya yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku ambayo pia huchangia katika kupunguza nguvu kazi ya taifa”, alisema  Dkt. Kisenge.

Akizindua taarifa hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF) Lutgard Kokulinda Kagaruki alisema tangu mwaka 2019 Tanzania imekuwa na matumizi makubwa ya tumbaku hali iliyosababisha nchi kuwekwa kwenye kundi la tahadhari la alama nyekundu inayoonyesha hatari.

Lutgard alisema Serikali iangalie namna ya kufanya marekebisho ya sheria na kupitisha muswada mpya wa sheria ya kudhibiti tumbaku nchini utakaoisaidia jamii kutokupata madhara yanayosababishwa na tumbaku.

“Kwa sasa sheria inayotumika ni ya mwaka 2003 ambayo haikidhi mahitaji ya wakati huu kwani udhaifu wake umechangia kuongezeka kwa matumizi ya tumbaku bila udhibit hali inayosababisha madhara makubwa kiafya”, alisema Lutgard.

Kwa upande wake Kiongozi wa Chama cha madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani Tanzania (APHYTA) ambaye pia ni daktari wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji Mwanaada Kilima alisema gharama za matibabu kwa watu wanaopata madhara yanayotokana na tumbaku ni kubwa na madhara hayo yamekuwa yakiwaathiri vijana zaidi.

“Tunatoa rai kwa vijana kupunguza au kuacha kabisa matumizi ya sigara na shisha kwani mgonjwa mmoja anayepata changamoto za mfumo wa upumuaji kutokana na matumizi ya tumbaku anaweza kutumia zaidi ya milioni nne kwa mwaka katika matibabu jambo ambalo ni hasara kwa taifa ikilinganishwa na faida ndogo ya shilingi bilioni mbili tu inayotokana na kilimo cha tumbaku inayopatikana nchini”, alisema Mwanaada.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi