Wafanyakazi JKCI Dar Group wapewa onyo dhidi ya ubadhilifu wa mali za Umma
Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali
ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa
taasisi hiyo wakati wa hafla ya
kuwatambua wafanyakazi bora kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi
Duniani.
Na JKCI
****************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group wametakiwa kuepuka ubadhilifu katika matumizi ya mali za
umma ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya vifaa vya ofisi pamoja na vitendo vya
uhujumu uchumi vinavyoweza kuathiri utendaji wa kazi za taasisi.
Rai hiyo imetolewa
jana na Mkurugenzi wa JKCI Hospitali ya Dar Group, Dkt. Tulizo Shemu
wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo kwa wafanyakazi bora ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani.
Dkt. Shemu alisisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kutumia
kwa uangalifu rasilimali za ofisi ili kupunguza upotevu wa fedha za umma na
kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
“Wewe Mfanyakazi usiwe chanzo cha upotevu wa mali za umma,
epuka kununua vifaa vya ofisi kwa gharama zisizo na sababu na hakikisha
unavitunza vizuri vifaa vyote vilivyonunuliwa.Ukibainika kufanya ubadhilifu au
matumizi mabaya ya mali za umma hatua za kinidhamu zitachukuliwa ikiwemo
kufikishwa TAKUKURU”, alisema Dkt.
Shemu.
Dkt. Shemu alisema kila mfanyakazi ana jukumu la kufanya kazi
kwa bidii na kuepuka uzembe ili kuendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa na
kuongeza kuwa uhujumu uchumi hauhusiani tu na wizi wa fedha bali pia ni pamoja
na kupokea mshahara bila kufanya kazi ipasavyo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Rasilimali Watu wa JKCI
Hospitali ya Dar Group Neema Minja, aliwapongeza wafanyakazi kwa ushirikiano
mzuri kazini na kuwataka kuongeza juhudi katika kuwahudumia wananchi kwa upendo
na weledi.
“Licha ya baadhi ya wafanyakazi kupata zawadi za wafanyakazi
hodarileo, nawasisitiza na nyie wengine kujituma kazini na kufanya kazi kwa
upendo ili wagonjwa waendelee kufurahia huduma zetu”, alisema Neema.
Nao baadhi ya wafanyakazi waliochaguliwa kuwa wafanyakazi
hodari wa mwaka wa fedha 2025/26
walisema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za pamoja na ushirikiano kazini.
Kwa upande wake Mhandisi wa Vifaa Tiba JKCI Dar Group
Elpidius Prosper ambaye ni mfanyakazi hodari wa hospitali hiyo kwa mwaka wa
fedha wa 2025/26 alisema ushindi huo ni motisha ya kuongeza juhudi zaidi kwani
wafanyazi wote ni bora katika nafasi zao hivyo basi wafanye kazi kwa bidii ili
wananchi waendelee kunufaika na huduma wanazozitoa.
“Kuchaguliwa kwangu kuwa meneja Tuzo hii ni matokeo ya
mshikamano wa wafanyakazi wote kwani kidole kimoja hakivunji chawa hivyo basi
tuendelee kushirikiana kwa bidii kwani kufanya kazi kwa pamoja kunaifanya
taasisi yetu ifike mbali zaidi”, alisema CPA. Ashura Ally, Meneja wa Kitengo
cha Fedha na Uhasibu wa JKCI Dar Group ambaye amechaguliwa kuwa meneja hodari
wa mwaka wa fedha wa 2025/26.
Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa JKCI Dar Group, John
Owenya ambaye amechaguliwa kuwa Mkuu wa
Kitengo hodari wa mwaka wa fedha 2025/26
alisema mafanikio ya kazi yanatokana na bidii na uwajibikaji wa kila
mmoja aliwahimiza wafanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi na matokeo yake yataonekana na watu kuridhika na
huduma unazozitoa.



Comments
Post a Comment