Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb) akionesha kitabu cha mwongozo wa upandikizaji moyo alichokizindua wakati wa hafla fupi ya kuzindua kitabu hicho iliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) akimkabidhi begi lenye vitendea kazi Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Hassan Mshinda baada ya kuzindua bodi hiyo katika viwanja vya JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) akimkabidhi begi lenye vitendea kazi Mjumbe wa bodi ya wadhamini wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo baada ya kuzindua bodi hiyo katika viwanja vya JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Hassan Mshinda  na wajumbe wa bodi hiyo mara baada ya kuizindua bodi hiyo katika viwanja vya JKCI iliyopo Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpatia tuzo ya kutambua mchango mkubwa anaoufanya katika sekta ya afya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) mara baada ya hafla ya uzinduzi wa Jengo la Utawala na Vipimo, Kitabu cha muongozo wa upandikizaji moyo na bodi ya wadhamini ya taasisi hiyo iliyofanyika katika viwanja vya JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Na JKCI

************************************************************************************************************

Katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za kibingwa bobezi nchini, Serikali kupitia Wizara ya Afya imezindua kitabu cha safari ya upandikizaji wa moyo nchini kuwasaidia wagonjwa ambao wanahitaji huduma hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho jijini Dar es Salaam Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha Sekta ya Afya kwa kutoa huduma za kibingwa bobezi katika matibabu moyo nchini.

“Niwapongeze JKCI kwa mpango huu ambao unaashiria hatua kubwa katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, kwasababu huduma hii ni kubwa sasa ni wakati wakuanza kuweka miundmbinu bora, mifumo ya kisheria pamoja na ushirikiano wa kimataifa”, alisema Mhe. Mchengerwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya upandikizaji wa moyo nchini kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Everist Nyawawa alisema watu milioni 64 duniani wenye matatizo ya moyo wanahitaji kupandikiziwa moyo ili waweze kuendelea kuishi.

Dkt. Nyawawa ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo alisema uhitaji wa kupandikiza mayo kwa wagonjwa wanaohitaji hudua hiyo inatokana na hatua za matibabu kwa wagonjwa wenye tatizo la moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure) ambao hulazimika kupatiwa matibabu ya muda mrefu na kutumia dawa mara kwa mara.

“JKCI tumeamua kuthubutu mambo yanayoonekana kuwa magumu ambayo yatawezekana kufanyika nchini ili kuokoa maisha ya watu wengi, hatua hii muhimu italisaidia taifa kupunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa wanaohitaji kupandikiza moyo nje ya nchi”, alisema Dkt. Nyawawa.

Dkt. Nyawawa alisema ili kufanikisha safari ya upandikizaji wa moyo nchini jamii inatakiwa kupewa elimu ya kutosha kuhusu huduma hiyo pamoja na kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Katika hatua nyingine Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa alizindua rasmi Bodi ya Wadhamini ya JKCI na kuitaka kuimarisha utawala bora na uwajibikaji pamoja na kusimamia vizuri Taasisi hiyo ili mikakati iliyowekwa iweze kutimizwa kwa wakati.

Akizindua bodi hiyo Mhe. Mchengerwa aliwataka wajumbe wa Bodi ya Wadhamini walioteuliwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kuwa kielelezo cha ubora katika huduma za moyo ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.



Comments

Popular posts from this blog

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi