Wafanyakazi JKCI wahimizwa kujifunza mbinu mpya kukuza huduma za moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Peter Kisenge akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakati wa kikao cha
wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa JKCI jijini Dar es
Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha akizungumza na wafanyakazi wa taasisi hiyo kuhusu
umuhimu wa kujaza taarifa zao za kazi katika mfumo wa PEPMIS wakati wa kikao
cha wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo jijini
Dar es Salaam.
Afisa Uhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Adamu Sembe
akitoa taarifa kuhusu fedha wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
*******************************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuwa wabunifu na wenye maono katika uotaji wa huduma kwa wananchi ili waweze kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kikao cha uwasilishwaji wa taarifa ya fedha kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika ukumbi wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kisenge alisema ili kutoa huduma bora zinazoendana na maendeleo ya teknolojia kuna ulazima kwa wafanyakazi kujifunza mbinu mpya za utendaji kazi na kuwa na maono ya mbali yatakayosaidia kuifanya taasisi hiyo kuwa kituo bora cha utaoaji wa huduma za moyo barani Afrika.
“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 tumefanikiwa kuimarisha mifumo kwa kutumia teknolojia ya kisasa, kwa sasa wagonjwa wanaweza kuweka miadi kupitia mtandao hivyo ni muhimu wafanyakazi wetu wawe na ubunifu na utayari wa kutumia tekinolojia za kisasa zinazotumia akili unde ili kufikia malengo tuliyojiwekea”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge aliongeza kuwa huduma za afya zimeendelea kuboreshwa katika taasisi hiyo kupitia ongezeko la vifaa tiba vya kisasa vilivyopo Hospitali ya JKCI Dar Group pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kufungua matawi katika maeneo mbalimbali ndani ya jiji la Dar es Salaam na mikoani ikiwemo Arusha na Chato.
“Tumefanikiwa kununua vifaa vya kisasa vya ECHO, machine za kisasa za matibabu ya mfumo wa chakula pamoja na kuboresha miundombinu hususani eneo la wagonjwa wa nje kusubiri huduma (OPD) katika Hospitali ya JKCI Dar Group”, alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasimali watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha alisema ni muhimu wafanyakazi kuzingatia taratibu zilizowekwa na Serikali katika utumishi wa umma hususani matumizi sahihi ya mfumo wa PEPMIS kwaajili ya tathmini ya utendaji kazi.
“Ni takwa la kisheria kwa watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii na kutumia mfumo wa PEPMIS kujaza majukumu yao ili waweze kufanyiwa tathimini itakavyosawasaidia katika maendeleo ya kazi ikiwemo kupanda madaraja na vyeo”, alisema Ghati.
Naye Afisa Uuguzi wa JKCI Dominick Kanani alisema utolewaji wa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi unawasaidia wafanyakazi kufahamu walipotoka, walipo na wanapokwenda hivyo kuwapa fursa ya kujipanga ili kuendana na malengo ya taasisi.
“Tutajituma zaidi katika kuwahudumia wananchi ili
kufikia malengo ya taasisi kwani ni taasisi pekee nchini inayotoa huduma za kibingwa
za moyo hivyo ni wajibu wetu kufanyakazi kwa bidii kwakuwa taifa linatutegemea”,
alisema Dominick





Comments
Post a Comment