Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi
Wahasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Ashura Ally na Edna Sanga wakifuatilia mada ya wakifuatilia mada ya kumbukumbu gani umeiacha katika eneo lako la kazi kutokana na matendo yako mazuri uliyoyafanya iliyokuwa inatolewa katika mkutano wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) unaofanyika jijini Arusha.
Wanachama wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) wakisubiri kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa wanachama wa chama hicho katika mkutano wao unaofanyika jijini Arusha.
*************************************************************************************************************************************************************************************************
Wanawake wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya za mioyo yao mara kwa mara ili kubaini mapema matatizo ya moyo na kuanza matibabu kabla hayajawa makubwa.
Wito huo umetolewa leo jijini Arusha na Daktari Bingwa wa Magonjwa
ya Moyo na Mkuu wa Kitengo cha Vipimo vya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI), Dkt. Engerasia Kifai
wakati akieleza huduma zinazotolewa na taasisi hiyo katika mkutano wa Chama cha
Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA).
“Ni muhimu kupima moyo mara kwa mara ili kubaini matatizo mapema
na kuepuka matatizo makubwa ya afya”, alisema Dkt. Kifai.
Dkt. Kifai alisema njia bora ya kuepuka magonjwa ya moyo ni
kuzingatia mtindo wa maisha wenye afya, ikiwemo kuepuka matumizi ya bidhaa za
tumbaku, kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kula chakula bora na kuepuka unywaji
wa pombe kupita kiasi.
“Katika ukuaji wa mwanamke, kuna mabadiliko mbalimbali ya ndani na
nje ya mwili ikiwemo kuongezeka kwa uzito na changamoto kwa moyo. Ni muhimu
kuzingatia vyakula unavyokula kwa kupunguza ulaji wa vyakula vya wanga, sukari
na chumvi kupita kiasi”, aliongeza Dkt. Kifai.
Akifafanua kuhusu huduma zinazotolewa na JKCI, Dkt. Kifai alisema
taasisi hiyo inatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na mishipa ya damu
kwa watoto na watu wazima, na imepanua huduma zake kwa kufungua kliniki katika
maeneo ya Kawe, Oysterbay, Dar Group na Chato.
“Taasisi yetu inafanya tafiti mbalimbali kuhusu magonjwa ya moyo, tunatoa
huduma za matibabu kwa wagonjwa waliopo majumbani, fiziotherapia, elimu ya
lishe bora na pia tunafanya upimaji wa afya kwa vikundi mbalimbali”, alisema.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo waliopata huduma ya upimaji wa
afya ya moyo waliipongeza JKCI kwa
huduma inayozitoa na kuomba huduma hiyo iendelee kutolewa katika mikutano
mingine.
“Nimepata huduma ya upimaji wa moyo na ushauri wa lishe. Huduma
imekuwa nzuri na ya haraka ninashukuru sana, ninawaomba wenzangu watumie
mkutano huu kujifunza mada mbalimbali zinazotolewa na kupima afya za miyo yao”,
alisema Pendo Mwakibinga kutoka EWURA.
“Nimefanyiwa vipimo vya sukari, presha, urefu na uzito, kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na mfumo wa umeme wa moyo. Nashukuru
kwani sasa najua hali ya moyo wangu , alisema Joyce Maduhu kutoka Benki ya Kilimo.
Huduma hizi za upimaji na ushauri wa magonjwa ya moyo zinazotolewa na JKCI katika mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa taasisi hiyo wa program yake ya kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo ijulikanayo kwa jina na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayowawezesha wananchi kupata mapema matibabu ya moyo.
Comments
Post a Comment