Wananchi wapata fursa ya vipimo vya moyo katika maonesho ya madini Geita

 Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mkazi wa Geita aliyefika katika banda la taasisi hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa katika maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika kwenye Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan  vilivyopo mjini Geita.

Afisa Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zabela Mkojera akichukua taarifa za mkazi wa Geita aliyefika katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo  mjini Geita.

*****************************************************************************************************************************************************************************************************************************

Wananchi wa mkoa wa Geita wameombwa kujitokeza kupata vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo Geita.

Wito huo umetolewa leo na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho hayo yanayoendelea mkoani Geita.

Dkt. Mayala alisema lengo la kushiriki kwenye maonyesho hayo ni kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kujua hali ya afya za mioyo yao na kupata msaada wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa bobezi mapema.

“Tumekuja Geita katika maonesho ya madini kwaajili ya kutoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo, tunawapima wananchi shinikizo la damu, kisukari, uzito na vilevile tunatoa elimu ya jinsi ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Dkt. Mayala.

Aliongeza kuwa mbali ya kutoa elimu ya afya wataalamu hao wameenda na vifaa vya kisasa vya kuchunguza moyo vitakavyotumika kuwapima wananchi jinsi mioyo yao inavyofanya kazi na kuhakikisha matatizo ya moyo yanabainika mapema.

“Tumekuja na vifaa ambavyo vinaangalia uwezo wa moyo kufanya kazi na kama kuna shida yoyote kwenye moyo tunatoa matibabu, tunatoa huduma hizi bure kwa lengo la kusaidia wananchi kupata uelewa wa afya zao”.

“Tunatoa wito  kwa wakazi wote walioko maeneo ya Geita na mikoa ya jirani waje kufanya vipimo vya moyo, ni vizuri kujua afya yako mapema na kuchukua hatua”, alisisitiza Dkt. Mayala.

Kwa upande wao wananchi waliojitokeza kupata huduma za vipimo na matibabu ya moyo walifurahishwa na huduma zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuomba serikali kuendeleza jitihada hizo katika maeneo mengine nchini.

“Ninashukuru nimepata huduma zote kuanzia vipimo vya awali mpaka vipimo vya moyo katika banda la JKCI, ninaiomba serikali iendelee kufanya hivi katika maeneo mbalimbali kwani itakuwa ni fursa ya kuwafikia watu wengi bila gharama”, alisema Hassan Omar Mkazi wa Mwanza.

“Nimekuja katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kupata huduma za vipimo na matibabu ya moyo, kiukweli huduma zao ni nzuri mpaka sasa hivi nasubiria kuelekea kwa daktari kwaajili ya tiba”, alisema Melesiana Malima mkazi wa Tambuka Reli Geita.

Huduma zinazotolewa na wataalamu wa JKCI katika Maonyesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini Geita ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo za kuhamasisha jamii kujikinga na magonjwa ya moyo kwa kupima afya zao mapema, kupata elimu na ushauri wa matumizi sahihi ya dawa za moyo.

Comments

Popular posts from this blog

Wateja wa CRDB kutibiwa JKCI kwa punguzo la asilimia 50%

Wanawake wa JKCI SACCOS wanaongoza kwa kumiliki hisa

JKCI, MOI NA MNH waitwa Comoro kutoa huduma za matibabu ya kibingwa