JKCI yagusa mioyo ya wanachama 125 wa TAWCA kupitia upimaji wa afya Jijini Arusha
Mwenyekiti wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) CPA. Mary Mabiti akimkabidhi jana Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Ashura Ally tuzo ya shukrani ya utoaji wa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanachama wa chama hicho waliohudhuria mkutano wa TAWCA unaofanyika jijini Arusha. Katika mkutano huo JKCI ilitoa bila malipo huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanachama 125.
Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Ashura Ally akigawa vipeperushi vya kutoa elimu ya magonjwa ya moyo jana kwa wanachama wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) waliofika katika banda la JKCI kwaajili ya kupata huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo inayotolewa katika mkutano wa TAWCA jijini Arusha.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Neema Matemba akitoa elimu ya lishe bora kwa mwanachama wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) aliyeshiriki mkutano wa chama hicho unaofanyika jijini Arusha. Katika mkutano huo JKCI ilitoa bila malipo huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanachama 125.
*****************************************************************************************************************************************************************************************************************
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanachama 125 wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) wanaoshiriki mkutano wa chama hicho unaofanyika jijini Arusha.
Mbali na upimaji huo unaofanyika bila malipo JKCI pia ilitoa elimu
kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo, ulaji wa lishe bora na matumizi
sahihi ya dawa za moyo kwa wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Daktari Bingwa wa Magonjwa
ya Moyo na Mkuu wa Kitengo cha Vipimo vya Moyo wa JKCI, Dkt. Engerasia Kifai alisema mwitikio umekuwa mkubwa jambo
linaloonyesha wananchi wengi sasa hivi wanaelewa umuhimu wa kupima afya zao
mara kwa mara.
“Tumewafanya vipimo vya sukari, shinikizo la damu, urefu na uzito
wa mwili, pamoja na vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na mfumo
wa umeme wa moyo (ECG). Tunafurahi kuona watu wamejitokeza kwa wingi, hii ni hatua
muhimu katika kujikinga na magonjwa ya moyo”.
“Kati ya watu 125 tuliowafanyia vipimo sita tumewaanzishia dawa za
shinikizo la juu la damu na wanne ambao walikuwa wanashida ya moyo
tumewabadilishia dawa za kutumia na kuwapa dawa ambao zinaendana na matatizo
waliyonayo ambazo naamini zitawasaidia”, alisema Dkt. Kifai.
Dkt. Kifai aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi pale
watakaposikia taasisi hiyo inafanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wananchi
kwani huduma hiyo inatolewa bila malipo ikiwa na lengo la kusogeza kwa karibu huduma
za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi.
“Wiki hii na wiki ijayo kuna wataalamu wenzetu wanafanya upimaji
katika maonesho ya madini yanayofanyika mkoani Geita, na katika kuadhimisha siku ya moyo duniani
tarehe 29 Septemba tutafanya upimaji Dar es Salaam katika hospitali yetu ya Dar Group iliyopo TAZARA. Ninawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi
kupima afya za mioyo yenu kwani huduma hii
tunaitoa bila malipo yoyote yale”, alisisitiza Dkt. Kifai.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania
(TAWCA) CPA. Tumaini Lawrence aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa
huduma ya upimaji na ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo wanayoitoa
kwa wanachama wa chama hicho na kuomba
ushirikiano uliopo kati yao uendelee.
“Wanawake wanakabiliwa na majukumu mengi ya kifamilia na mara
nyingine hukosa muda wa kupima afya zao, wanaweza kuwa na dalili za ugonjwa
fulani lakini wakaona ni sawa na kutokwenda hospitali kwa wakati.Tunaishukuru
JKCI kwa huduma mnayoitoa tunaomba mshirikiane nasi ili wanawake wengi zaidi
wapate fursa ya kupima na kujua afya zao mapema”.
“Kwa wanachama ambao hawajafanikiwa kupima ninawaomba watenge muda
wakapime kwa kuwa afya ya moyo ni kipaumbele cha kila mmoja wetu”, alisema CPA.
Tumaini.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo walieleza kufurahishwa na
mpangilio mzuri wa utoaji wa huduma na kusema kuwa imewapa uelewa na hamasa ya
kuendelea kujali afya zao.
Huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za JKCI za kuhamasisha jamii kujikinga na magonjwa ya moyo kupitia upimaji wa mapema, utoaji wa elimu ya afya na ushauri wa kitabibu.
Comments
Post a Comment