JKCI na SACH kuokoa maisha ya watoto 20 Zambia kwa kufanya upasuaji wa moyo
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) wakiwa katika kikao cha kujadili watoto watakaofanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya siku sita ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayoanza leo katika Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).
Na JKCI
***********************************************************************************************
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Okoa
Moyo wa Mtoto la nchini Israel (SACH) kufanya kambi maalumu ya upasuaji wa moyo
kwa watoto 20 wa nchini Zambia.
Kambi hiyo ya siku sita inaanza leo katika Hospitali ya Taifa
ya Moyo ya nchini Zambia (NHH) kwa kushirikiana na wataalamu wa Hospitali hiyo,
na daktari wa usingizi kutoka nchini Ethiopia.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana nchini Zambia Daktari
bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Godwin Sharau alisema katika kambi hiyo utafanyika upasuaji wa kufungua
kifua pamoja na upasuaji wa tundu dogo kwa
kutumia mtambo wa Cathlab.
“Kambi hii inafanyika kwa kushirikiana na wataalamu kutoka
nchini Tanzania, Zambia, Ethiopia, na Israel wote tukiwa na lengo la kuwasaidia
watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo nchini Zambia”, alisema Dkt. Godwin
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto
(SACH) la nchini Israel Simon Fisher alisema Shirika hilo limeandaa kambi hiyo
kuwasaidia wataalamu wa afya wa nchini Zambia na kuwajengea uwezo katika kutoa
huduma za matibabu ya moyo kwa watoto.
Simon alisema JKCI, na SACH wamekuwa na ushirikiano wa muda
mrefu tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 hivyo kupitia ushirikiano
huo wamepanga kwa pamoja kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo nchini
Zambia.
“SACH imeweza kuwajengea uwezo madaktari bingwa wa magonjwa
ya moyo kwa watoto wa JKCI kwa kipindi cha muda mrefu, na baadaye kuanza
kuwajengea uwezo wataalamu wa Hospitali ya Moyo Zambia hii yote ni kuhakikisha
huduma bingwa bobezi za magonjwa ya moyo kwa watoto zinapatikana katika nchi
hizi”, alisema Simon
Comments
Post a Comment