Watoto 28 wafanyiwa upasuaji wa moyo, Serikali yaokoa milioni 270

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akikabidhi tuzo ya shukrani kiongozi wa timu ya watalaamu kutoka King Salman Humanitarian Aid and Relief Center nchini Saudi Arabia Aijohara Hamza wakati wa hafla fupi ya kufunga kambi ya upasuaji wa moyo kwa watoto iliyofanyika JKCI. Taasisi hiyo iliishukuru King Salman Humanitarian Aid and Relief Center kutokana na ushirikiano walionao wa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na matibabu ya moyo kwa watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi zawadi Naibu Balozi wa Saudi Arabia Abdallah Kashani wakati wa hafla fupi ya kufunga kambi ya upasuaji wa moyo kwa watoto iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa King Salman Humanitarian Aid and Relief Center kutoka Saudi Arabia. Watoto 28 walifanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Abdallah Kilima, Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Abdallah Kashani na watalaamu kutoka King Salman Humanitarian Aid and Relief Center wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kufunga kambi ya upasuaji wa moyo kwa watoto iliyofanyika JKCI.
**********************************************************************************************************************************************************************************************************
Serikali imeokoa kiasi cha shilingi milioni 270 kupitia kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka King Salman Humanitarian Aid and Relief Center nchini Saudi Arabia.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo hivi karibuni
jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema mafanikio
hayo yametokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia chini
ya uongozi mahili wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema kwa muda wa siku nane wamefanya upasuaji wa moyo kwa watoto waliokuwa
na matatizo ya matundu kwenye moyo, kurekebisha vyumba vya moyo na mishipa ya
damu ya moyo na kuokoa maisha yao.
“Watoto wote wanaendelea vizuri wataruhusiwa siku chache
zijazo baada ya hali zao kuimarika, tunawashukuru wenzetu wa kituo cha King
Salman Humanitarian Aid and Relief cha nchini Saudi Arabia licha ya kutoa
huduma ya upasuaji wa moyo wamekuja pia na vifaa tiba ambavyo vimetumika katika
matibabu ya watoto hawa”,alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania
Abdallah Kashani aliishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wanaowapa na
kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (
JKCI) kwa watoto wenye matatizo ya moyo kama sehemu muhimu ya kutoa huduma za
kibinadamu kwa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo,
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Balozi
Abdallah Kilima alisema serikali inaunga mkono jitihada zinazofanywa na
wataalamu wa upasuaji wa moyo kutoka nchini Saudi Arabia.
“Shukrani ziende kwa
mfalme wa Saudi Arabia na madaktari ambao wamekuwa tayari kuja Tanzania kufanya
upasuaji wa moyo kwa watoto upasuaji ambao ni mgumu kufanyika na kuchukuwa muda
mrefu lakini tumeona kuna upasuaji umechukuwa muda mfupi na tunashuhudia
mafanikio makubwa”, alisema Balozi Kilima.
Naye Kiongozi wa Timu
ya watalaamu kutoka Kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief cha
nchini Saud Arabia Aijohara Hamza alisema mafanikio waliyoyapata ya kuwatibu
watoto yametokana na ushirikiano mzuri wanaoupata kutoka kwa watalaamu wenzao
wa JKCI na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali ya Tanzania katika taasisi
hiyo.
“Tunamshukuru Mungu tumefanikiwa kuwafanyiwa upasuaji wa moyo
watoto 28 na wote wametoka salama kwani ni furaha yetu sisi kuona tunaokoa maisha
ya watoto na kurudisha tabasamu kwenye
familia zao”, alisema Dkt. Aijohara.
Wazazi wa watoto ambao wametibiwa katika kambi hiyo waliwashukuru
wataalamu hao kwa kuokoa maisha ya
watoto wao baada ya kuteseka kwa muda mrefu na ugonjwa wa moyo uliokuwa
unawasumbua.
“Mtoto wangu aligundulika kuwa na matatizo ya moyo miaka
miwili iliyopita na niliambiwa matibabu yake yatagharimu kiasi cha shilingi milioni
tisa lakini nimelipia shilingi milioni moja fedha zingine nimepata msamaha wa
matibabu na mtoto amefanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri”, alisema Mwaija
Juma.
“Namshukuru Mungu mwanangu amepona peke yangu nisingeweza kabisa kumudu gharama za matibabu lakini nawashukuru madakatari, wauguzi na wataalamu wote wa afya kwa kurejesha furaha kwangu na kwa mtoto wangu”, alisema Asha Omar.
Comments
Post a Comment