Elimu ya Shinikizo la juu la damu yatolewa katika maonesho na madini Geita
Afisa Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Makrina Komba akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyetembelea banda la hiyo lililopo katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mjini Geita.
Afisa Utafiti na Mafunzo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zabela Mkojera akimpima urefu na uzito mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mjini Geita.
Tatizo la ugonjwa wa shinikizo la
damu waelezwa kuongezeka kwa vijana huku idadi kubwa ya vijana hao kuishi na tatizo
hilo bila ya kuonyesha dalili zozote.
Hayo yamesema na daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala wakati
wa maonesho ya nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika
Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo mjini Geita.
Dkt. Mayala alisema kulingana na
takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni
1.3 duniani wanaishi na ugonjwa wa shinikizo la damu huku asilimia 46 ya watu
hao wana umri wa kuanzia miaka 25.
“Wananchi wanatakiwa kupima afya zao
mara kwa mara ili kujua kama wana tatizo la shinikizo la damu, na kwa wale
waliopimwa na kukutwa na ungonjwa huu wanatakiwa kupimwa mara tatu kwa siku tatu
tofauti kuthibitisha kuwa wana ugonjwa huo,” alisema Dkt. Mayala.
Dkt. Mayala aliongezea kuwa watu
wengine hupata dalili kama vile uchovu usio wa kawaida, jasho jingi, na maumivu
ya kichwa sehemu ya nyuma ya kichogo lakini bado utawakuwa hawafuatilii afya
zao.
“Asilimia kubwa ya watu wenye
shinikizo la damu mara nyingi hawana dalili, tafiti zinaonyesha kati ya
wagonjwa kumi wagonjwa sita wana tatizo la shinikizo la damu na wagonjwa hawa
wapo ambao wanajijua na wengine hawajijui,” alisema Dkt. Mayala.
Dkt. Mayala alisema kuna haja ya
kuwekeza kwenye elimu ya afya kwa jamii ili kuondoa mitazamo potofu na kukuza
utamaduni wa kupima afya mara kwa mara hasa kwa wale ambao hawana dalili zozote
lakini wako kwenye hatari.
Baadhi ya wananchi waliotembelea
banda la Taasisi hiyo walishukuru kwa kupata elimu na kuona umuhimu wa kufanya
uchunguzi wa afya zao mara kwa mara.
“Nimepata elimu ya kutosha kuhusu
shinikizo la juu la damu, ninawashukuru madaktari kwa kutupa elimu hii muhimu,”
Alisema Nelson Simon Mkazi wa Geita.
“Madaktari wamenifundisha kuhusu
ulaji bora kuepuka matumizi ya chumvi nyingi na umuhimu wa mazoezi ili
kuepukana na magonjwa ya moyo,” Alisema Laurencia Bujashi mkazi wa Geita.



Comments
Post a Comment