HTAF na Vodacom kushirikiana kusaidia matibabu ya Moyo kwa watoto wenye mahitaji
Mtendaji Mkuu Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire wakibadilishana hati ya mkataba wa ushirikiano wa kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team
Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip
Besiimire wakionesha hati ya mkataba wa ushirikiano wa kusaidia watoto wenye
magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo
katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa
JKCI Dkt. Peter Kisenge
Mtendaji Mkuu Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani akimuelezea huduma zinazotolewa katika kliniki ya watoto wenye magonjwa ya moyo Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo wakati wa kusaini hati ya mkataba wa ushirikiano wa kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela akimuonesha mmoja wa watoto
waliopatiwa huduma katika Taasisi hiyo Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip
Besiimire alipotembelea JKCI leo wakati wa kusaini hati ya mkataba wa
ushirikiano wa kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika
Taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire
wakimsikiliza Daktari bingwa wa wagonjwa wa dharura na mahututi wa JKCI Vivian
Mlawi walipotembelea wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kabla
ya kusaini hati ya mkataba wa ushirikiano na Taasisi isiyo ya Serikali ya Heart
Team Africa Foundation (HTAF) kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo leo jijini
Dar es Salaam.
Na JKCI
***************************************************************************************************
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF)
kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania
zimesaini hati ya makubaliano maalumu ya kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto
nchini hususan wale wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo wanaotibiwa
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI).
Makubaliano hayo yaliyosainiwa leo jijini Dar
es Salaam yanahusisha kusaidia matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo na
kukarabati wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).
Akizungumza katika hafla ya kusaini
makubaliano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
aliipongeza Vodacom kushiriki katika kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo na
kuunga jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha matibabu ya moyo
yanapatikana nchini.
“Ushirikiano huu utasaidia sana kuwafikia
watoto wenye magonjwa ya moyo wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu lakini
pia utasaidia kukarabati wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU)
hivyo kuongeza nafasi ya kutoa huduma,” alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema takwimu zinaonesha kuwa
kati ya watoto 10,000 huzaliwa
nchini wakiwa na matatizo ya moyo kila mwaka, ambapo zaidi ya
4,000 huhitaji upasuaji wa haraka.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Heart Team Africa
Foundation (HTAF) Dkt. Naizi Majani alisema mkataba wa HTAF na Vodacom umelenga
kuhakikisha kuwa watoto wanaotoka katika familia duni wanapata huduma za
matibabu JKCI.
“Lengo letu ni kuwasaidia watoto wenye
magonjwa ya moyo ambao wengi wao hukosa msaada ukilinganisha na watu wazima
ambao hupata msaada kutoka kwa watu wengi wanaowazunguka, hivyo makubaliano yetu
ni kuhakikisha tunarudisha furaha kwa watoto ambao wanapitia maumivu makali
yanayotokana na maradhi ya moyo”, alisema Dkt. Naiz.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire alisema Vodacom imefanya
tathmini na kuona kuwa gharama za matibabu hazipaswi kuwa kikwazo cha kuokoa
maisha ya watoto hivyo ikaamua kushirikian na HTAF kuokoa maisha ya watoto
wanaohitaji upasuaji wa moyo.
“Tupo hapa leo kuiunga mkoni Serikali ya
Tanzania kwa kusaidia watoto 150 wenye magonjwa ya moyo kupata matibabu na
kurejesha matumaini kwa familia zao kwani kila mtoto anastahili nafasi ya
kuishi bila kujali uwezo wa familia zao”, alisema Besiimire.
Kupitia makubaliano hayo HTAF na Vodacom
wanatarajia kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za upasuaji wa moyo kwa
watoto nchini, hatua itakayosaidia kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya
moyo kwa watoto.
Comments
Post a Comment