Raia wa Malawi avutiwa na huduma bora za moyo JKCI, atoa shukrani za dhati


Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda akizungumza na mgonjwa kutoka nchini Malawi Dinnot-Phiri aliyetibiwa katika taasisi hiyo hivi karibuni ambaye alishukuru kwa huduma bora za matibabu ya moyo alizozipata. Kushoto ni Mratibu wa Utalii Tiba wa taasisi hiyo Salome Mbunga.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda akimpa zawadi mgonjwa kutoka nchini Malawi Dinnot-Phiri aliyetibiwa katika taasisi hiyo hivi karibuni ambaye alishukuru kwa huduma bora za matibabu ya moyo alizozipata.
***********************************************************************************************************************************************************************
Mkazi wa Blantyre nchini Malawi Enita Dinnot-Phiri ameishukuru Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma bora za kiwango cha kimataifa za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa watanzania na wasio watanzania .
Shukrani hizo amezitoa
hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kufurahishwa
kwake na huduma za matibabu ya moyo alizozipata katika taasisi hiyo.
Enita alisema mara baada
ya kugundulika kuwa na tatizo la moyo alipewa nafasi ya kuchagua nchi ya kwenda
kutibiwa ikiwemo India lakini yeye alichagua kwenda Tanzania katika Taasisi ya
Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) mahali ambapo amepata matibabu ya kiwango cha
juu.
“Nilifika hapa Jumamosi
iliyopita na nilijua kwamba huenda
nikapatiwa matibabu siku za kazi yaani kuanzia Jumatatu, lakini baada tu ya
kupokelewa kutoka Airport nilianza kupatiwa matibabu ambayo kwakweli
sikutarajia kuyapata nimefurahi sana”.
“Namshukuru Mungu nimepata
matibabu na nimeruhusiwa, ninawapongeza wafanyakazi wote wa taasisi hii kwa moyo wao wa ukarimu na upendo kwani kazi
yao wanayoifanya ya kuokoa maisha ya watu ni kubwa na wanastahili kupewa
pongezi”, alishukuru Enita.
Kwa upande wake Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dickson Minja
alisema walimpokea Enita kutoka nchini Malawi ambaye alikuwa na changamoto ya
moyo iliyohitaji kupata huduma ya matibabu ya haraka.
Dkt. Minja alisema kutokana
na uhitaji wa haraka wa huduma ya matibabu kwa mgonjwa huyo siku ya Jumapili kwa
kutumia mtambo wa Cathlab walimfanyia upasuaji wa moyo wa bila kupasua kifua ambao
ulikwenda vizuri bila ya changamoto yoyote.
“Ninawaomba wananchi wenye matatizo ya moyo wafike katika taasisi yetu ili wapate matibabu kwa wakati kwani muda wote hata siku za sikukuu tunatoa huduma za matibabu ya viwango vya ubora wa kimataifa hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali yetu kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Comments
Post a Comment