JKCI yatua Hospitali ya ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road (KRPRRH) kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo
Askari polisi wa kambi ya Kilwa Road, familia zao na wananchi wa Temeke wakiwa katika foleni ya kupatiwa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyofanyika katika kambi hiyo katika kuadhimisha miaka 10 ya JKCI.
Afisa Takwimu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Makrina Komba akimpima kiwango cha sukari kwenye damu askari polisi wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na Taasisi hiyo katika kuadhimisha miaka 10 ya JKCI.
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa
Kilwa Road (KRPRRH) Gema Marandu akimpima shinikizo la damu mwananchi wa Temeke
aliyefika katika kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo
ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba Mkoba iliyokuwa ikifanywa
na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuadhimisha miaka 10 ya Taasisi
hiyo.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nanta-Aimee
Wambali akimsikiliza askari polisi wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya
uchunguzi wa magonjwa ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
tiba Mkoba iliyokuwa ikifanyika katika kambi ya Polisi ya Kilwa Road katika
kuadhimisha miaka 10 ya JKCI.
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa
Kilwa Road (KRPRRH) Donatha Kisaka akimpima urefu na uzito mwananchi wa Temeke
aliyefika katika kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo
ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba Mkoba iliyokuwa ikifanywa
na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuadhimisha miaka 10 ya Taasisi
hiyo.
Picha na JKCI
********************************************************************************************************************
Askari Polisi, familia zao na wananchi 172 wamefanyiwa
uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya siku mbili ya
matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba.
Kambi hiyo imefanyika hivi karibuni katika Hospitali ya Rufaa
ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road (KRPRRH) katika kuadhimisha miaka 10 ya Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu ilipoanzishwa mwezi Septemba mwaka 2015.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo Mganga Mfawidhi
wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road (KRPRRH) Dkt. Nyanda
Lushina alisema hospitali hiyo imefanya ushirikiano na JKCI katika kutoa huduma
za uchunguzi wa magonjwa ya moyo ili kwa pamoja waweze kuwafikishia huduma za
kibingwa askari polisi, familia zao na wananchi wanaotibiwa katika hospitali
hiyo.
“Hospitali yetu ilianzishwa kwaajili ya kuwatibu askari
polisi na familia zao lakini sasa hivi imekuwa kimbilio la wananchi ambao
wanatuzunguka, hivyo tukaona tufanye ushirikiano na JKCI ili tuwarahisishie
kupata huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Nyanda
Upimaji huu umetoa nafasi kwa watumishi wetu wanaokuwa kazini
muda mrefu na kusahau kufanya uchunguzi wa afya yakiwemo magonjwa ya moyo, lakini
pia kupitia nafasi hii wananchi wanaotuzunguka wamepata nafasi ya kufahamu afya
zao.
Dkt. Nyanda aliomba mbeleni JKCI wawe na mahusiano na vituo
vya afya vya Polisi vilivyopo katika kila mkoa waweze kufikisha huduma za
kibingwa za moyo na kuhakikisha kuwa afya za askari polisi zipo vizuri katika
kulinda usalama wa nchi.
Kwa upande wake daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Daud Gwilenza alisema JKCI inatimiza miaka 10 kwa kutoa huduma za
uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa makundi mbalimbali yakiwemo askari polisi,
wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“Mwitikio katika kambi hii umekuwa mkubwa, askari polisi wamejitokeza
kwa wingi na walikuwa tayari kufanyiwa uchunguzi ambapo tumeweza kuwaelimisha
kuhusu afya ya moyo na waliokuwa tayari tumewapima moyo”, alisema Dkt. Daud
Dkt. Daud alisema katika kambi hiyo askari polisi, familia
zao na wananchi wameweza kupimwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography),
shinikizo la damu, sukari kwenye damu, uwiano wa urefu na uzito pamoja na
vipimo vya damu.
Naye mwananchi aliyepata huduma katika kambi hiyo ambaye
hakutaka jina lake lifahamike alisema huduma za uchunguzi wa moyo zifanyike
mara kwa mara katika Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road
(KRPRRH) kuwasaidia wananchi wengi wa maeneo ya Temeke wanaoitumia hospitali
hiyo.
“Hospitali ya Rufaa ya Polisi ngazi ya Mkoa Kilwa Road
(KRPRRH) inatusaidia sana sisi wananchi wa Temeke, tukiweza kupata huduma za
kibingwa kama hizi za moyo itatusaidia kupata huduma kirahisi na kwa haraka
pale zinapohitajika”, alisema mwananchi huyo.
Comments
Post a Comment