Wafanyakazi 149 wa JKCI Hospitali ya Dar Group wapata ajira serikalini
Mkuu wa Kitengo cha Utawala wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joachim Asenga akitoa mafunzo ya wajibu wa mtumishi wa umma kwa wafanyakazi 149 waliokuwa chini ya hospitali binafsi ya Tanzania Occupational Health Services (TOHS - Dar Group) kabla haijakabidhiwa kwa JKCI Novemba 2022 ambao wote wamepata ajira serikalini Agosti mwaka huu.
.jpg)
Mchunguzi Mkuu Kiongozi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ilala Nerry Mwakyusa akitoa elimu ya madhara ya rushwa mahali pa kazi kwa wafanyakazi 149 waliokuwa chini ya hospitali binafsi ya Tanzania Occupational Health Services (TOHS - Dar Group) kabla haijakabidhiwa kwa JKCI Novemba 2022 ambao wote wamepata ajira serikalini Agosti mwaka huu.
Kabla ya kukabidhiwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) wafanyakazi hao walikuwa chini ya
hospitali binafsi ya Tanzania Occupational Health Services (TOHS - Dar Group).
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Idd Lemah wakati akifungua mafunzo
elekezi ya siku tatu kwa watumishi
waliopata ajira ya kudumu serikalini.
Lemah alisema serikali iliwapatia
Hospitali ya Dar Group iliyopo wilayani Temeke kuwa sehemu ya JKCI. Kuwepo kwa
hospitali hiyo kumetatua changamoto ya nafasi ambayo walikuwa wanakabiliana
nayo kwa muda mrefu na kusaidia kuboresha huduma za matibabu wanazozitoa kwa wananchi.
“Serikali ilitukabidhi hospitali hii ikiwa na majengo, mali, watumishi na madeni. Baada ya
kufanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi tumeweza kuwaajiri wafanyakazi wote na leo
tunatoa mafunzo haya ili kuhakikisha wanazingatia
sheria, taratibu, weledi na maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kuepekana na vitendo vya rushwa”.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wafanyakazi hawa na kuwapatia ajira ninaamini
walivyokuwa wanatoa huduma bora wakati wako katika sekta binafsi wataendelea kutoa
huduma hiyohiyo serikalini”, alisema Lemah.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Utawala wa Taasisi ya
Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Joachim Asenga alisema mafunzo hayo ya siku tatu kwa
wafanyakazi hao yamelenga kuwajengea mbinu bora za uwajibikaji katika kazi zao za kila siku.
“Kutolewa kwa mafunzo haya ni takwa la kisheria kwa watumishi
waliopata ajira serikalini, watafundishwa mada mbalimbali zikiwemo za madhara
ya rushwa mahali pa kazi, haki na wajibu wa mtumishi katika utumishi wa umma, na
Usalama wa Taifa”, alisema Asenga.
Akizungumza wakati akitoa mada ya madhara ya rushwa mahali pa
kazi Mchunguzi Mkuu kiongozi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
mkoa wa Ilala Nerry Mwakyusa alisema kutolewa kwa mafunzo kuhusiana na rushwa kutawasaidia waajiriwa wapya kutambua madhara ya rushwa
mahali pa kazi na jinsi ya kuiepuka.
“Dhana ya kwamba wale wanaotoa rushwa ya fedha ndiyo
wanaoweza kupata huduma katika sekta ya afya ni kinyume cha sheria na inaweza
kusababisha vifo kwa watu watakaoshindwa
kutoa fedha kwani watachelewa kupata huduma ambayo ingeokoa maisha yao”,
alisema Nerry.
Nao wafanyakazi waliohudhuria
mafunzo hayo walishukuru kwa nafasi waliyoipata ya kupata ajira Serikalini na
kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa na wananchi wanaowahudumia.
“Tunashukuru tangu tumekabidhiwa kwa JKCI maslahi yetu
yameboreshwa na tumeajiriwa serikalini, tutaendelea kutoa huduma za kizalendo
kuhakikisha matokeo makubwa yanaonekana na kuifanya hospitali hii kuwa ya mfano
wa kuigwa” alishukuru Daktari Bingwa wa magonjwa yatakanayo na kazi Elias
Birago.
“Kabla sijaajiriwa serikalini ilinilazimu kila baada ya muda fulani kujaza fomu za mkataba wa ajira kitu ambacho kilikuwa kinaniletea mawazo kwani kuna wakati unafikiria kama unaweza kupata mkataba au la. Ninashukuru kwa ajra niliyoipata na ninaahidi kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora zaidi”, alisema Afisa Tehama Mary Vyabula.
Comments
Post a Comment