JKCI yazindua mfumo wa kidigitali wa miadi ya wagonjwa
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Fiona Kavishe akionesha tovuti yenye mfumo wa kidigitali wa
miadi mtandao.
Na JKCI
*********************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha mifumo
miwili ya kisasa ya kuweka miadi kwa ajili ya kumuona daktari na mfumo wa namna
ndugu wa mgonjwa anavyoweza kumtembelea mgonjwa aliyelazwa hospitalini.
Mifumo hiyo inapatikana kupitia tovuti rasmi ya taasisi hiyo
(www.jkci.or.tz) ambapo wagonjwa sasa wanaweza kuweka miadi ya kumuona daktari
kwa urahisi kwa kubofya sehemu ya Appointments na kuchagua tarehe, muda pamoja
na aina ya huduma wanayohitaji.
Akizungumzia mfumo huo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Fiona Kavishe alisema uanzishwaji wa
mfumo huo umelenga kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuongeza ufanisi katika
utoaji wa huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo.
“Faida ya mfumo wa
miadi ya kumuona daktari utamsaidia wananchi kumuona daktari yoyote anayemtaka
tofauti na awali ilikuwa wagonjwa baadhi wanamuona daktari huyo huyo”, alisema
Fiona
Fiona alisema kupitia mfumo wa kutembelea wagonjwa waliolazwa
wodini, ndugu wa wagonjwa wanaotaka kuwatembelea wagonjwa waliolazwa
hospitalini wanaweza kutumia mfumo huo kwa kubofya sehemu ya Visitor kuchagua
tarehe ya kuwatembelea wagonjwa na kufuata taratibu zilizowekwa.
Kwa upande wake Daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe
Mwinchete alisema mfumo huo utawarahisishia madaktari kupanga ratiba zao vizuri
na kuweza kufahamu kwa siku wana idadi ya wagonjwa wangapi tofauti na awali
ilikuwa ngumu kwao kuweka ratiba zao vizuri.
Dkt. Salehe alisema wagonjwa wakitumia mfumo wa miadi ya
kumuona daktari kutasaidia kupunguza malalamiko ya wao kukaa muda mrefu
hospitali kusubiri huduma lakini pia kutawapa muda wa kupumzika na kuacha tabia
ya kuamka mapema kuwahi foleni ya kumuona daktari.
Naye mgonjwa aliyefanikiwa kufanya miadi kupitia tovuti hiyo
Wenceslous Shoo alisema mfumo huo ni mzuri na una faida nyingi kwa wagonjwa
kwani watakuwa na muda mchache wa kukaa hospitali.
“Huduma hii ya kuweka miadi mtandaoni ni mzuri kwasababu
inapunguza usumbufu wa kupanga foleni na kuamka alfajiri sana, ningeomba elimu
itolewe na kuwafikia watu wengi zaidi ili waweze kuutumia mfumo huu” alisema
Shoo.
Mfumo wa kidigitali wa kuweka miadi ya kumuona daktari na
kutembelea wagonjwa waliolazwa JKCI umeanzishwa ili kuimarisha huduma kwa
wananchi, kuongeza uwazi na kuhakikisha usalama wa wagonjwa walipoko wodini kwa
kudhibiti idadi ya wageni.
Comments
Post a Comment