Matibabu ya moyo nchini yageuka neema: Bilion 172 zaokolewa


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpatia tuzo Mhe. Albert Msando kwa niaba ya Rais mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 10 ya JKCI iliyofanyika jana katika hoteli ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpatia zawadi mgeni rasmi wa hafla ya kutimiza miaka 10 ya JKCI Mhe. Albert Msano jana wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam 

Mkurugenzi wa Shirika la Save a Child Heart (SACH) la nchini Israel Simon Fishers akimpatia zawadi iliyotolewa na Shirika hilo  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla ya kutimiza miaka 10 ya Taasisi hiyo iloyofanyika jana katika hotel ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa kamati ya maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naiz Majani akitoa taarifa ya nini kimefanyika katika maadhimisho hayo jana wakati wa hafla ya kutimiza miaka 10 ya JKCI iliyofanyika katika hoteli ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam.


Mgeni rasmi wa hafla ya kutimiza miaka 10 ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mhe. Albert Msando akikata utepe kuzindua kitabu cha miaka 10 ya Taasisi hiyo jana katika hoteli ya Serena iliyopo jijini  Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendani wa JKCI Dkt. Peter Kisenge

Na JKCI

*********************************************************************************************************************

Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa kiasi cha bilioni 172 ambazo zilikuwa zinatumika kupeleka wagonjwa wa moyo nje ya nchi.

Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa wilaya ya Ubungo Mhe.  Albert Msando kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 10 ya utoaji wa huduma za matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyofanyika katika Hoteli ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mhe. Msando alisema taifa limeshuhudia kupungua kwa matumizi ya fedha za kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa muda wa miaka 10 tangu mwaka 2015 wakati Serikali ilipoanzisha Taaisi hiyo kutoa huduma bingwa bobezi za moyo.

“Serikali ya awamu ya sita kupitia Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kuwekeza vifaa tiba vya kisasa kurahisisha na kutoa matibabu kuendana na  technolojia" alisema Mhe. Msando

Mhe. Msando aliwataka wataalamu wa afya kufanya tafiti ambazo zitatumia lugha rahisi na kuwafikia watu wa kawaida na wadau mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kwa miaka 10 mfululizo taasisi hiyo imejikita katika kutoa huduma bingwa za matibabu ya moyo kwa kutibu wagonjwa wa ndani ya nje ya nchi.

"Kwa sasa JKCI siyo tu ni Hospitali ya Tanzania bali ya Africa kwani wagonjwa kutoka nchi za Afrika na nje ya Afrika kama India, Uturuki, China, Ufaransa, Ujerumani, wanatibiwa hapa, hivyo kuifanya JKCI kuikomboa Afrika kwenye masuala ya Moyo”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema kwa kipindi cha miaka 10 Taasisi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji wa moyo bila kufungua kifua ambayo ni mafanikio makubwa sana katika matibabu ya moyo. 

"JKCI tumeweza kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimesaidia katika kuleta mafanikio ya taasisi, pia tumeajiri watumishi waliokuwa wanafanya kazi  Hospitali ya Dar Group ambayo sasa ni tawi la JKCI", alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema JKCI imetoa huduma za tiba mkoba kwa kuifikia mikoa 16 ya Tanzania na kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo wananchi ambao wengi wao wasingeweza kuzifuata huduma mahali zilipo.

Naye mwenyekiti wa kamati ya maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI Dkt. Naiz Majani alisema katika maadhimisho hayo JKCI ilifanya shughuli mbalimbali katika jamii ikiwa ni sehemu ya maadhimisho.

Dkt. Naiz alisema JKCI imeza kuwafikia wanafuzi, askari polisi na wananchi kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa kuadhimisha miaka 10 ya JKCI.

"Tulianza kuadhimisha miaka 10 ya JKCI kwa kuzindua kamati ya maandalizi ya upandikizaji wa moyo ili Taasisi yetu nayo iweze kutoa huduma kubwa ya matibabu ya moyo kama ambavyo hospitali kubwa duniani zinafanya", alisema Dkt. Naiz

Dkt. Naiz alisema sambamba na hilo JKCI katika kuadhimisha miaka 10 imeweza kuwakutanisha wataalamu wa afya na wanafunzi wa elimu ya sekondari kujadili kuhusu utalii tiba na namna ambavyo matibabu ya moyo yanaenda kuleta utalii tiba nchini.

"Wataalamu wa afya kutoka hospitali mbalimbali nchini waliweza kushiriki katika mdahalo wa kisayansi na kubadilishana ujuzi wakati huu tukiadhimisha miaka 10 ya JKCI", alisema Dkt. Naiz

Hafla hiyo ya maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI yenye kauli mbiu  tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele imeonyesha kuwa mwanzo wa mafanikio makubwa zaidi katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini na kuzifanya huduma hizo kuwa sahemu ya utalii nchini.


Comments

Popular posts from this blog

Wateja wa CRDB kutibiwa JKCI kwa punguzo la asilimia 50%

Wanawake wa JKCI SACCOS wanaongoza kwa kumiliki hisa

JKCI, MOI NA MNH waitwa Comoro kutoa huduma za matibabu ya kibingwa