Mwitikio mkubwa wapelekea JKCI kuongeza siku mbili za upimaji wa Moyo bila malipo
Wananchi waliofika katika Hospitali ya JKCI-Dar Group iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke wakisubiri kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani yanayofanyika katika hospitali hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya JKCI-Dar Group iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani yanayofanyika leo.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shem akiwaeleza wananchi
waliofika katika hospitali hiyo iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke huduma za
matibabu wanazozitoa wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani yanayofanyika leo ambapo
hospitali hiyo inatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo bila malipo kwa
wananchi.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingindo akitoa elimu ya lishe kwa mwananchi aliyefika katika Hospitali ya JKCI-Dar Group iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo katika maadhimisho siku ya moyo duniani yanayofanyika leo.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Happines Shirima akimpima shinikizo la damu na mapigo ya moyo mwananchi aliyefika katika hospitali hiyo iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo bila malipo zinazotolewa katika maadhimisho siku ya moyo duniani yanayofanyika leo.
***********************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeongeza siku mbili zaidi za upimaji bure wa afya ya moyo, hatua iliyochukuliwa kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza kupima na kupata ushauri wa kitabibu katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani.
Mkurugenzi
wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema awali upimaji huo ulikuwa umepangwa
kufanyika kwa siku moja katika Hospitali ya Dar Group lakini kutokana na idadi
kubwa ya wananchi waliojitokeza, taasisi imeamua kuongeza muda ili kuhakikisha
watu wengi zaidi wanapata nafasi ya kupimwa.
“Tumeona
mwamko mkubwa wa wananchi. Kwa siku leo tumewahudumia watu 232. Ili kutimiza
dhamira ya kuelimisha na kuzuia magonjwa ya moyo, tumeongeza siku mbili ili
wananchi wengi zaidi wapate huduma hizi muhimu”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt.
Kisenge alibainisha kuwa takwimu zinaonyesha watoto 10,000 huzaliwa nchini
wakiwa na matatizo ya moyo kila mwaka, ambapo zaidi ya 4,000 huhitaji upasuaji
wa haraka. Kwa watu wazima changamoto kubwa zinatokana na ulaji usiozingatia
lishe bora, kutokufanya mazoezi, uvutaji sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi
na magonjwa nyemelezi kama kisukari na shinikizo la damu.
Dkt.
Kisenge alisema JKCI inaendelea na kampeni yake ya upimaji na matibabu ya
magonjwa ya moyo kwa wananchi ijulikanayo kwa jina la Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan Outreach Services ambayo tayari imeshafika katika mikoa 23
na kuwafikia zaidi ya watu 23,000 kwa kutoa elimu na huduma za upimaji na
matibabu ya moyo.
Dkt.
Kisenge aliwataka Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha, ikiwemo kufanya
mazoezi, kula vyakula vyenye lishe bora na kupima afya mara kwa mara ili
kulinda afya ya moyo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa JKCI-Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alisema gharama za
matibabu ya moyo ni kubwa, hivyo wananchi wanapaswa kujikinga mapema kwa
kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ili kama watakutwa na matatizo ya moyo
waanze matibabu mapema kabla ya changamoto hazijawa kubwa.
“Kuzibua
mshipa wa moyo hugharimu zaidi ya Sh milioni 6, na kifaa cha kusaidia umeme wa
moyo kinaweza kugharimu hadi Sh milioni 10. Njia rahisi na nafuu zaidi ni
kuzuia ugonjwa kabla haujawa mkubwa”, alisema Dkt. Shemu.
Naye
Daktari Bingwa wa Moyo kwa Watoto wa JKCI-Dar Group Eva Kuganda alisema katika
kambi hiyo wanafanya upimaji kwa watoto na kuwaomba wazazi wenye watoto wawapeleke
kupima afya zao.
“Katika
upimaji wa watoto umeonyesha baadhi yao wana matatizo ya moyo bila kuwa na
dalili zozote. Hii inaonyesha umuhimu wa vipimo mapema ili matatizo
yashughulikiwe kabla hayajawa makubwa”, alisema Dkt. Eva.
Kwa
upande wa wananchi waliojitokeza kupima afya za mioyo yao, wengi walieleza
kuridhika na huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kuelewa hali ya afya
zao pia elimu waliyopewa ya matumizi sahihi ya dawa, jinsi ya kuutunza moyo na
lishe bora wataitumia katika maisha yao ya kila siku.
“Kwa sisi wananchi
ambao hatuwezi kumudu gharama za upimaji, JKCI imeturahisishia sana. Tungeomba
serikali iendelee kuipa nguvu taasisi hii ili iweze kutoa elimu na matibabu kwa
wananchi wasiojiweza,” alisema Kassim Likaukwa, mkazi wa Temeke.
“Nilikuwa nikitembea kidogo moyo wangu unaenda kasi, lakini baada ya upimaji na maelezo niliyopata hapa, nimeweza kuelewa hali yangu na kuanza kuchukua tahadhari za kiafya”, alisema Grace Shirima mkazi wa Tegeta.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Usipuuze Mapigo ya Moyo: Zingatia kinga, uchunguzi wa mapema na maisha yenye afya”.
Comments
Post a Comment