Spika wa Umoja wa Bunge la Visiwa vya Comoro apongeza uwekezaji wa Tanzania katika huduma za afya hususan matibabu ya moyo
Spika wa Umoja wa Bunge la Visiwa vya Comoro Mhe.
Moustadroine Abdou akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alipotembelea Kliniki ya JKCI
Oysterbay kwaajili ya kuona huduma zinazotolewa pamoja na kupata matibabu.
Spika wa Umoja wa Bunge la Visiwa vya Comoro Mhe.
Moustadroine Abdou ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwekeza kikamilifu
katika sekta ya afya na kuimarisha huduma za kibingwa hususan matibabu ya moyo.
Ametoa pongezi hizo hivi karibuni alipotembelea Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia Kliniki yake ya Oysterbay ambako alishuhudia
huduma zinazotolewa na pia kupata matibabu.
Mheshimiwa Moustadroine alisema amevutiwa na miundombinu ya
kisasa iliyowekezwa katika taasisi hiyo, akibainisha kuwa inakidhi viwango vya
kimataifa katika kutoa huduma za matibabu ya kibingwa.
“Nimefurahi leo nimetembelea JKCI Kliniki ya Oysterbay na
kujionea namna ambavyo Serikali ya Tanzania imewekeza katika vifaa vya kisasa
vya matibabu ya moyo na kuwasomesha wataalamu. Nimepata huduma bora na kugundua
kuwa wataalamu wa afya hapa ni marafiki wazuri wa wagonjwa”, alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa JKCI Dkt. Angela Muhozya
alisema taasisi hiyo imeendelea kutoa huduma za kibingwa kwa Watanzania na
wageni kutoka mataifa mbalimbali jambo linaloonesha dhamira ya Serikali ya
Tanzania katika kuokoa maisha na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya
nchi.
“Tunajivunia kuona viongozi wa kimataifa wakitembelea JKCI na
kushuhudia huduma tunazotoa. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wa Tanzania na
jirani wanapata huduma bora za moyo kwa gharama nafuu na mazingira rafiki”,
alisema Dkt. Anjela.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo itaendelea kusomesha wataalamu na
kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuhakikisha huduma zinabaki kuwa za
kiwango cha juu kimataifa.
Kwa mujibu wa Spika Moustadroine, Tanzania imeweka mfano bora
wa uwekezaji katika afya ambao unaweza kuigwa na mataifa mengine barani Afrika.
Comments
Post a Comment