JKCI yawataka Wafamasia kutoa dawa kwa kufuata maelekezo ya Madaktari


Mkurugenzi wa Idara ya magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kuadhimisha siku ya wafamasia duniani iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Famasia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Wellu Kaali akielezea umuhimu wa wafamasia katika jamii wakati wa hafla fupi ya kuadhimisha siku ya wafamasia duniani iliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo.


Baadhi ya wafamasia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza wakati wa hafla fupi ya kuadhimisha siku ya wafamasia duniani iliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Idara ya magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akikata keki wakati  akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge katika hafla fupi ya kuadhimisha siku ya wafamasia duniani  iliyofanyika jana katika taasisi hiyo.

Picha na JKCI

***************************************************************************************************************

Wafamasia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuhakikisha wanatoa dawa kwa wagonjwa wenye maelekezo ya madaktari pekee ili kusaidia jamii kuachana na tabia ya kutumia dawa bila ushauri wa kitaalamu.

Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Dkt. Tatizo Waane wakati akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge katika hafla fupi ya kuadhimisha Siku ya Wafamasia Duniani.

Dkt. Waane alisisitiza kuwa katika taaluma ya famasia hakuna kitu kinachoitwa dawa ya nusu dozi, hivyo wafamasia wanapaswa kuwahudumia wagonjwa kwa kuzingatia usahihi wa maelekezo yaliyotolewa na daktari.

“Ni wajibu wenu kufanya kazi kwa kuzingatia utaalamu na maadili ya taaluma yenu. Hivi ndivyo mtakavyosaidia kuokoa maisha ya jamii, hasa ikizingatiwa kuwa wapo watu wanaopenda kupata huduma bila kufuata taratibu za kitabibu”’alisema Dkt. Waane.

Aidha aliongeza kuwa wafamasia wakifuata maadili ya kazi yao watakuwa na nafasi kubwa ya kuokoa maisha na kujenga imani ya wananchi katika huduma za afya zinazotolewa.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Famasi wa JKCI Wellu Kaali alisema wafamasia ni nguzo muhimu katika mnyororo wa huduma za afya kwani wanahusika moja kwa moja na usimamizi wa upatikanaji, uhifadhi na usahihi wa matumizi ya dawa na vifaa tiba.

Wellu alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, JKCI imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa za moyo zinazookoa maisha ya watoto na watu wazima.

Aliongeza kuwa idadi ya famasi imeongezeka kutoka moja hadi nane, huku huduma mpya zikianzishwa ikiwemo famasi ya wagonjwa maalumu (VIP patients), uzalishaji wa dawa za watoto na vitendanishi.

“Tunajivunia mchango wetu katika kuongeza matumizi sahihi ya dawa na kutoa huduma bora, hatua inayoiweka JKCI katika nafasi ya kuwa kitovu cha umahiri wa huduma za moyo Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara”, alisema Wellu.

Siku ya Wafamasia Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Septemba, ikilenga kuonyesha mchango wa taaluma ya famasia katika kuboresha huduma za afya. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Unapofikiria Afya, Mfikirie Mfamasia”.

 


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo