JKCI yapokea msaada wa vifaa vya fiziotherapia vyenye thamani ya shilingi milioni 24
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Physiocare Tanzania Remla Shirima akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani msaada wa Ultrasound therapy kwaajili ya kuwahudumia wanamichezo kupitia programu ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo Sports Cardiology leo jijini Dar es Slaam. Kampuni za Physiocare Tanzania na Enovis ya Afrika Kusini zimetoa msaada wa vifaa vya kutoa huduma za fiziotherapia kwa wanamichezo vyenye thamani ya shilingi milioni 24.

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Kampuni ya Physiocare Tanzania na Enovis ya Afrika Kusini wakiangalia utiwaji wa saini wa makubaliano ya ushirikiano wa kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wanamichezo kupitia program ya Sports Cardiology uliokuwa unafanyywa na viongozi wa taasisi hizo leo jijini Dar es Salaam.
************************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea msaada wa vifaa tiba vya kutolea huduma ya fiziotherapia kwa wanamichezo vyenye thamani ya shilingi milioni 24 kutoka kampuni za Physiocare Tanzania na Enovis ya Afrika Kusini.
Pamoja na kupokea msaada huo leo jijini Dar es Salaam taasisi
hizo pia zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa kutoa huduma za upimaji na
matibabu ya moyo kwa wanamichezo kupitia
program ya Sports Cardiology.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani alisema kusainiwa kwa makubaliano hayo kutawasaidia wanamichezo kupata huduma
bora za upimaji na matibabu ya moyo.
“Ninashukuru sana kwa msaada mliotupatia, kuwepo kwa vifaa
hivi vya kisasa vya fiziotherapia vinavyotumia umeme kutawasaidia wanamichezo watakaopata
matatizo ya moyo baada ya kufanyiwa upasuaji kuendelea na matibabu ya
fiziotherapia.
“JKCI kupitia washirika
wetu kama vile Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunahakikisha afya
za wanamichezo zinakuwa salama kwa kuwafanyia uchunguzi kabla ya kuingia katika
mashindano mbalimbali na hivyo kuweza kugundua matatizo ya moyo kwa wanamichezo
mapema kabla hawajapata madhara”, alisema Dkt. Naizihijwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Physiocare
Tanzania Remla Shirima alisema wameshirikiana na kampuni ya Enovis ya Afrika Kusini katika
kusaini makubaliano ya ushirikiano na JKCI kwa kuwatambua watu wanaojihusisha
na michezo pamoja na kufanya mazoezi.
“Tunathamini kile kinachofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa wanamichezo, na kwa
kutoa vifaa hivi vya fiziotherapia bila shaka vitaboresha na kusaidia huduma za
utengamao kuwa bora na za kisasa zaidi”, alisema Remla.
Akizumzia kuhusu ushirikiano huo Mkurugenzi Mkuu wa kampuni
ya Enovis ya Afrika Kusini Pieter Verwey alisema wanathamini kile kinachofanywa na Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete katika kuimarisha afya za wanamichezo kwa kuwafanyia
uchunguzi kabla hawajaumwa anaamini vifaa hivyo vya teknolojia ya kisasa vitasaidia kuimarisha na kuboresha huduma za
matibabu ya moyo hapa nchini.
Naye Mratibu wa Sports Cardiology kutoka JKCI Hospitali ya Dar Group Daktari bingwa wa magonjwa
ya moyo Eva Wakuganda alisema kusainiwa
kwa makubaliano hayo ni kwa muhimu kutokana na hatari iliyopo kwa
wanamichezo ya kudondoka ghafla na kupoteza maisha wakati wanafanya mazoezi au
wakati wa mashindano kutokana na mabadiliko yanayoweza kutokea ndani ya mioyo
yao.
“Baadhi ya wanamichezo wamekuwa wakikumbana na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo au matatizo ya moyo ambayo hayajawahi kujulikana kwahiyo hatua hii ni muhimu sana katika kuboresha afya za wanamichezo”, alisema Dkt. Eva.
Comments
Post a Comment