Jengo la Utawala na Vipimo lenye thamani ya Tshs Bilioni 9.7 lazinduliwa kuimarisha huduma za moyo nchini
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa na Mwenyekiti wa bodi
ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Hassan Mshinda
wakizindua jengo la Utawala na Vipimo wakati wa hafla fupi ya kuzindua jengo
hilo iliyofanyika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini
Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa akiangalia moja ya
mashine inayotumia akili unde kufanya uchunguzi wa afya wakati wa hafla fupi ya
uzinduzi wa jengo la Utawala na Vipimo iliyofanyika jana katika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa akiangalia moja ya mashine inayotumia akili unde kufanya uchunguzi wa afya wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa jengo la Utawala na Vipimo iliyofanyika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya figo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Frida Moyo akimuelezea Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa huduma
zinazotolewa katika kitengo cha Dialysis wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa jengo
la Utawala na Vipimo iliyofanyika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Afisa Uhusiano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes
Sikaonga akifanya mahojiano na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengera
alipotembelea Studio ya Health Promotion wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa
jengo la Utawala na Vipimo iliyofanyika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokelewa na mtoto
aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipowasili katika
Taasisi hiyo kwaajili ya hafla fupi ya kuzindua jengo la Utawala na Vipimo iliyofanyika
jana jijini Dar es Salaam.
Picha na
JKCI
****************************************************************************************************
Serikali kupitia Wizara ya Afya imezindua rasmi Jengo la Utawala na Vipimo lililopo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) hatua inayolenga kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini.
Akizungumza katika
hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam Waziri wa Afya Mhe. Mohamed
Mchengerwa, alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za afya na
kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa kuelekea mwaka 2050.
“Jengo hili limegharimu
takribani shilingi bilioni 9.7, litasaidia kuongeza uwezo wa JKCI kwenye
uchunguzi, matibabu na usimamizi wa huduma za moyo, kwani thamani yake halisi
ipo katika maisha yatakayookolewa, tabasamu litakalorejeshwa kwa jamii na ubora
wa huduma utakaoongezeka”, alisema Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa alisema
kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi iliyopita JKCI imeweza kutoka kuwa ndoto ya
kuwa kituo cha kisasa cha moyo hadi taasisi inayotambulika kimataifa kwa huduma
za uchunguzi, upasuaji wa moyo, mafunzo ya wataalamu na tafiti za kisayansi.
Mhe. Mchengerwa alisema
jengo alilolizindua lina maabara ya kisasa iliyogharimu kiasi cha shilingi
bilioni 5.4, yenye uwezo wa kufanya vipimo vya magonjwa ya moyo, damu, figo,
homoni na kemia ya mwili kwa viwango vya kimataifa, hivyo kuboresha usahihi wa
uchunguzi na matibabu.
“Maabara hii pia
imefungwa teknolojia ya Akili Unde (AI) na mifumo ya kisasa ya Automation
inayorahisisha uchakataji wa sampuli, kuongeza usahihi wa majibu na kupunguza
muda wa kusubiri matokeo ya vipimo”, alisema Mhe. Mchengerwa
Aidha Mhe. Mchengerwa
alisema jengo hilo pia linatoa huduma za vipimo vya Echocardiography (ECHO),
X-Ray za kisasa, kliniki ya wagonjwa wakimataifa, kitengo cha Dialysis huku
likiwa na studio ya uhamasishaji na uelimishaji wa afya (Health Promotion
Studio) kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma juu ya kinga ya magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya
moyo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema uwepo wa jengo hilo ni sehemu ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaotibiwa
katika taasisi hiyo kwani watafanyiwa uchunguzi vizuri kupitia maabara hiyo na
kupatiwa matibabu stahiki.
Dkt. Kisenge alisema
JKCI imekuwa kutokana na huduma inazozitoa kwani sasa Taasisi hiyo ni miongoni
mwa Taasisi kubwa Afrika Mashariki na Kati kufanya upasuaji wa moyo mkubwa
ikiwemo upasuaji wa kisasa wa kubadilisha valvu ya moyo bila kufungua kifua (Transcatheter
Aortic Valve Implantation - TAVI).
“Tumefungua matawi ya
JKCI maeneo mbalimbali hapa Dar es Salaam na mkoani Arusha, tunataka miaka 10
ijayo kila mkoa uwe na tawi la JKCI, lakini pia tunafikiria kufungua tawi la
JKCI nje ya nchi yote haya ni kuionesha dunia kuwa JKCI tumeendelea katika
kutoa huduma bingwa bobezi za moyo”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge
alisema maono ya JKCI katika miaka ijayo ni kuhakikisha kuwa inafanya upasuaji
wa moyo kwa kutumia roboti lakini pia inaweza kupandikiza moyo kwa wagonjwa
wanaohitaji huduma hiyo.






Comments
Post a Comment