Mkutano wa CardioTan Imaging 2026 Kujadili Matumizi ya Akili Unde matibabu ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na
waandishi wa habari leo kuhusu Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo
– CardioTan Imaging 2026 utakaofanyika tarehe 4 hadi 6 mwezi Juni mwaka huu
katika ukumbi wa Blue Sapphire Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Mkutano wa
nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026, Iddi Lemah
akizungumza na waandishi wa habari leo kuelekea mkutano huo utakaofanyika
tarehe 4 hadi 6 mwezi Juni mwaka huu katika Ukumbi wa Blue Sapphire jijini Dar
es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa
ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Engerasia Kifai
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa Mkutano wa Nne wa
Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026 utakaofanyika tarehe 4
hadi 6 mwezi Juni mwaka huu katika Ukumbi wa Blue Sapphire jijini Dar es
Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya
magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ubora wa Mkutano wa Nne wa Kimataifa
wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026 utakaofanyika tarehe 4 hadi 6 mwezi
Juni mwaka huu katika Ukumbi wa Blue Sapphire, Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa
kamati ya maandalizi ya Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo –
CardioTan Imaging 2026 wakifuatilia mada zilizokuwa zikiendelea katika mkutano
na waandishi wa habari kuelekea mkutano
huo utakaofanyika tarehe 4 hadi 6 mwezi Juni mwaka huu katika Ukumbi wa Blue
Sapphire jijini Dar es Salaam.
Na JKCI
***************************************************************************************************
Mkutano
wa nne wa kimataifa wa magonjwa ya moyo (CardioTan Imaging 2026) kuwakutanisha
wataalamu wa afya kutoka nchi mbalimbali duniani kujadili matumizi
ya teknolojia za kisasa katika utambuzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Mkutano huo unaofanyika katika
Ukumbi wa Blue Sapphire jijini Dar es Salaam utafanyika kwa siku tatu kuanzia
tarehe 4 hadi 6, 2026 kwa lengo la kubadilishana ujuzi, kuboresha huduma za
uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo pamoja na kuongeza ushirikiano wa
wataalamu kutoka nchi washiriki wa mkutano huo.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema mkutano huo ni sehemu ya
jukwaa la wataalamu wa afya kubadilishana uzoefu na kujadili mbinu mpya za
utambuzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kutumia akili unde.
“Katika mkutano huu
tutajadiliana njia mbalimbali za kutibu magonjwa ya moyo na miongoni mwa mada
zitakazojadiliwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa hususani akili
unde (Artificial Intelligence) katika kutibu magonjwa ya moyo”, alisema Dkt.
Kisenge.
“Tunategemea madaktari wa
moyo pamoja na wataalamu wa radiolojia kuanzia ngazi ya diploma hadi wale wenye
utaalamu wa hali ya juu watakaa pamoja kujadili njia mbalimbali za kutumia
teknolojia za kisasa kuwasaidia wagonjwa wa moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema mkutano
huo utatumika pia kama sehemu ya kuitangaza Tanzania kimataifa lakini pia
kutangaza utalii tiba unaofanya na Taasisi hiyo.
“Mkutano huu vilevile
unaenda kuchangia katika masuala ya tiba utalii kwa sababu kutakuwa na
wawakilishi kutoka nchi mbalimbali za Afrika watakaokuja kujionea uwezo wa JKCI
na maendeleo makubwa yaliyofanyika katika Taasisi yetu”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo (CardioTan Imaging 2026)
Iddi Lemah alisema mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada za JKCI kutoa mafunzo
kwa wataalamu wa afya na wadau wengine wa sekta ya afya.
“Mkutano huu ni wa nne
tangu tulipoanzisha mpango huu wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wa
afya, watunga sera na wadau wengine, tunawakaribisha wataalamu na wadau mbalimbali
kushiriki mkutano huu na kujionea mafanikio tuliyoyapata”, alisema Lemah.
Akielezea namna mkutano
huo utakavyokuwa Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema mkutano huo pia
utawawezesha wataalamu wa afya kujadili umuhimu wa kugundua magonjwa ya moyo
katika hatua za awali.
“Moja ya mada
zitakazojadiliwa katika mkutano huu ni
ile ya namna ya kufanya utambuzi wa magonjwa ya moyo katika hatua za awali na
jinsi vipimo mbalimbali vinavyoweza kusaidia matibabu ya wagonjwa wa moyo”, alisema
Dkt. Waane.
Naye Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Engerasia Kifai
alisema kupitia mkutano huo kutafanyika uzinduzi wa chama cha umoja wa upimaji
moyo kuwaunganisha wataalamu hao na kubadilishana uzoefu.
“Siku hiyo pia kutakuwa
na uzinduzi wa chama cha umoja wa upimaji moyo Tanzania (Echocardiography
Society) tukiwa na lengo la kuwajumuisha na kuwasajili wataalamu wote
wanaofanya vipimo vya moyo na kusaidia kutoa mafunzo endelevu, kuongeza wigo wa
tafiti ili kuboresha huduma za utambuzi wa magonjwa ya moyo”, alisema Dkt.
Kifai.
Mkutano wa CardioTan Imaging 2026 unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano, kujadili, kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kutoa huduma bingwa bobezi za matibabu ya moyo na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha huduma bingwa za magonjwa ya moyo barani Afrika.





Comments
Post a Comment