JKCI yahamasisha wananchi Dodoma Kujua Namba Zao na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza
Mkurugenzi wa Idara ya
Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati
Chacha akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakati wa
maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali
Park vilivyopo jijini Dodoma.
Meneja Mkuu wa Shirika
la Masoko ya Kariakoo CPA. Ashraph Abdulkarim akisaini kitabu cha wageni
alipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho
ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park
vilivyopo jijini Dodoma.
Meneja Mkuu wa Shirika
la Masoko ya Kariakoo CPA. Ashraph Abdulkarim akizijua namba zake kwa kupima
uwiano wa urefu kwa uzito alipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika
Viwanja vya Chinangali Park vilivyopo jijini Dodoma.
Afisa Utafiti wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Makrina Komba akimpima mzunguko wa kiuno
mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park vilivyopo
jijini Dodoma.
Afisa Uuguzi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Edna Kajuna akimuonesha betri za moyo (peacemaker)
mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park vilivyopo
jijini Dodoma.
Na JKCI
****************************************************************************************************
Wananchi wa mkoa wa Dodoma na mikoa jirani wametakiwa kutumia maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kufanya uchunguzi wa afya na kuzijua namba zao ili waweze kuwa salama na kujilinda na magonjwa yasiyoambukiza.
Rai hiyo imetolewa na
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Daud Gwilenza wakati wa
maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park vilivyopo jijini
Dodoma.
Dkt. Daud alisema JKCI
kwa kushirikiana na Wizara ya Afya inafanya kampeni ya Jua Namba Zako ikiwa na
lengo la kupunguza magonjwa yasiyoambukiza katika jamii kwa kuifanyia jamii
uchunguzi wa afya wa mapema na kuwapa elimu ambayo itawalinda na magonjwa
yanayoweza kuepukika.
“Ni jukumu letu
kuhakikisha kuwa jamii inakuwa salama na inasaidiwa ili iweze kuyafahamu
magonjwa yasiyoambukiza, kufahamu namna ya kujikinga na magonjwa hayo lakini
pia kwa wale ambao tayari wamepata magonjwa hayo tunawapa nafasi ya kufuatilia
afya zao ili wasipate madhara zaidi”, alisema Dkt. Daud
Dkt. Daud alisema kuwa
watu wengi wamekuwa wakiogopa kufanya uchunguzi wa afya kwa kuhofia kuwa
wakikutwa na magonjwa yasiyoambukiza watapata mtikisiko na kupoteza muelekeo
jambo ambalo si la kweli kwani mtu anapogundulika mapema inamsaidia kujua namna
ya kuishi, vitu vya kuacha na nini cha kufanya ili asipate madhara zaidi.
Kwa upande wao wananchi
waliopata huduma katika banda la Taasisi hiyo wameipongeza JKCI kwa kuendelea
kusogeza huduma hizo karibu na wananchi na kuwapunguzia adha ya kuzifuata
mahali zilipo.
Dorcas Judica mkazi wa
Dodoma alisema JKCI ni Taasisi ambayo ipo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa
huduma inazozitoa zinawafikia watanzania wote ndio maana imekuwa ikifanya kambi
za matibabu katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
“Kwakweli Taasisi zote
za afya zioneshe nia kama ambavyo JKCI inafanya kutufikishia huduma bingwa bobezi
karibu na kutusaidia, kwani jamii yote inatamani kujijua na kuchukua hatua za
haraka za kujikinga na magonjwa hayo”, alisema Dorcas
Dorcas alisema uoga wa
watu kufanya uchunguzi wa afya unasababishwa na hali duni ya maisha, watu
wanakuwa na hofu wakikutwa na magonjwa kama ya moyo watawezaje kumudu gharama
za matibabu lakini hawajui kuwa wangejijua mapema ingewasaidia kutotumia
gharama nyingi kuyatibu.
Naye Ibrahimu Muimba
alisema jamii ikiifahamu vizuri kampeni ya Jua Namba Zako na ikachukua hatua
itasaidia kupunguza magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo hivyo
kujenga Taifa lenye afya bora.
“Leo nimepata elimu ya
umuhimu wa kufahamu shinikizo langu la damu, kiwango cha sukari kwenye damu,
uwiano wangu wa urefu kwa uzito, mapigo yangu ya moyo na kiwango cha mafuta
kwenye damu, yote haya kama nitajilidha nisiyapate basi nitakuwa salama na
mwenye afya”, alisema Ibrahimu
Comments
Post a Comment