TAKUKURU yachangia milioni 20.89 matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo.



 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akipokea hundi ya shilingi milioni 20.89 kutoka kwa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala Faustine Maijo kwaajili ya kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.



 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea hundi ya shilingi milioni 20.89 kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala Faustine Maijo akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 20.89 kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Msimamizi wa Wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tedy Tarimo akielezea namna wodi hiyo inavyotoa huduma wakati Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala Faustine Maijo alipotembelea wodi hiyo mara baada ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 20.89 kuchangia gharama za matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

*********************************************************************************************************************************************

Na Mwandishi Maalumu-Dar es Salaam.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imechangia shilingi milioni 20.89 kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Fedha hizo zimekabidhiwa katika Shirika lisilo la kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) linalounga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kuchangisha fedha za matibabu ya moyo kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo hasa watoto wenye magonjwa ya moyo.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea hundi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI kupitia HTAF imekuwa ikiratibu upatikanaji wa fedha kwaajili ya kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo pamoja na kuendeleza tafiti na elimu kuhusu magonjwa hayo.

Dkt. Kisenge alisema HTAF imekuwa daraja muhimu la kuwahusisha wadau mbalimbali katika kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo na kuimarisha elimu pamoja na tafiti za magonjwa hayo hivyo kubadilisha maisha ya watoto wengi waliokuwa katika hali ngumu kiafya.

 “Moja ya kazi inayofanywa na Shirika hili ya HTAF ni kukusanya rasilimali fedha lakini vilevile kusimamia masuala ya tafiti na elimu kuhusu magonjwa ya moyo ambayo yanachangia vifo vingi duniani, mwaka jana tulikusanya bilioni 2.7 na tumeweza kuwasaidia watoto zaidi ya 305 wenye matatizo ya moyo kufanyiwa upasuaji bila kulipia gharama za matibabu”, alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirila lisilo la Kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naizihijwa Majani alisema licha ya Serikali kubeba sehemu kubwa ya gharama za matibabu ya moyo bado familia nyingi zinashindwa kumudu gharama ndogo iliyobakia katika huduma hizo bingwa za matibabu ya moyo hivyo ikaona ishiriki ili watoto wapate matibabu kwa wakati.

“Matibabu ya moyo ni miongoni mwa matibabu yenye gharama kubwa sana duniani hata baada ya Serikali kuchangia sehemu kubwa ya gharama bado kuna gharama nyingi zinahitajika kukamilisha matiababu kwa baadhi ya magonjwa ya moyo”,

“Tunawashukuru TAKUKURU kwa kutushika mkono kwa sababu fedha hizi zimetoka mifukoni mwa wafanyakazi wa TAKUKURU wakiwa na lengo la kuwasaidia watoto wanaohitaji matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Naizihijwa.

Naye Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala Faustine Maijo alisema taasisi hiyo imeguswa na changamoto zinazowakabili watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na familia zao na kuamua kurudisha kwa jamii kwakuchangia matibabu yao.

“Tunatambua kuwa mtoto mwenye tatizo la moyo anahitaji matibabu ya haraka na gharama zake mara nyingi ni kubwa kwa wazazi wengi, mchango huu mdogo ukawe faraja na ufungue mlango wa matibabu kwa baadhi ya watoto wanaoendelea kupata matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)”, alisema Maijo.

Akitoa neno la shukrani Meneja Mkuu kutoka Global Medicare Daniel Lazaro aliishukuru TAKUKURU kwa kuonesha mfano bora wa uwajibikaji kwa jamii kupitia msaada huo.

“Uongozi wa TAKUKURU umeweza kuwashirikisha watumishi wake katika jambo muhimu la kusaidia wahitaji kwenye jamii, huu ni mfano wa kuigwa kwa sababu si taasisi nyingi zenye utamaduni wa kujitolea kusaidia watu wenye mahitaji maalum kama ambavyo mmefanya”, alisema Lazaro.

Mchango huo wa shilingi milioni 20.89 unatarajiwa kuwasaidia watoto wengi zaidi wenye matatizo ya moyo kupata matibabu ya kibingwa yanayotolewa na JKCI katika kurejesha tabasamu lililofichwa na maumivu ya magonjwa ya moyo yanayowakabili.

 Picha na JKCI





Comments

Popular posts from this blog

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi