Benki ya KCB yachangia shilingi milioni 20 matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akipokea hundi ya
shilingi milioni 20 kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Vihatarishi na Uzingatiaji benki
ya Kenya Commercial (KCB) tawi la Tanzania Angelina Semioni jana wakati wa
hafla fupi ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo iliyofanyika
katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akielezea namna wodi
ya watoto wenye magonjwa ya moyo inavyotoa huduma wakati wa hafla fupi ya
kukabidhi hundi ya
shilingi milioni 20 iliyotolewa na benki ya Kenya Commercial (KCB) kwaajili ya
watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo iliyopo jijini
Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea hundi ya shilingi milioni 20 kutoka benki ya Kenya Commercial (KCB) tawi la Tanzania kwajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha
Vihatarishi na Uzingatiaji kutoka Benki ya Kenya Commercial (KCB) tawi la
Tanzania Angelina Semion akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi hundi ya
shilingi milioni 20 kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo
wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es
Salaam.
Na JKCI
**************************************************************************************************
Benki ya Kenya
Commercial (KCB) tawi la Tanzania imechangia kiasi cha Shilingi milioni 20
kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza wakati wa
hafla fupi ya kupokea hundi kutoka benki hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema benki hiyo imetumia
falsafa ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na upendo na kuleta
matumaini kwa watoto wenye uhitaji wa matibabu ya moyo.
“KCB wamefanya tendo
jema la upendo kwa kuwapa watoto wenye magonjwa ya moyo matumaini na kuleta
faraja katika familia zinazopitia changamoto ya kuuguza watoto hao kwa muda
mrefu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema changamoto
kubwa inayoongeza idadi ya magonjwa ya moyo kwa watoto nchini ni pamoja na wazazi
kutokuwa na uelewa kuhusu magonjwa hayo hivyo kuishi maisha yanayoweza
sababisha magonjwa ya moyo ikiwemo kula lishe duni hasa wakati wa ujauzito,
unywaji wa pombe uliokithiri, matumizi ya sigara, na wakati mwingine magonjwa
hayo husababishwa na vina saba.
“Asilimia kubwa ya watoto
wenye magonjwa ya moyo wanatoka katika falimia zisizokuwa na uwezo wa
kugharamia matibabu, Serikali yetu imekuwa mstari wa mbele kuwasaidi watoto
wenye magonjwa hayo kwa asilimia 70 na asilimia 30 iliyobaki inatolewa na
Taasisi pamoja na wadau mbalimbali”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge aliongezea
kuwa JKCI ni Taasisi pekee yenye uwezo wa kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto
400 ndani ya mwaka mmoja katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati, na
kuainisha kuwa gharama za matibabu hayo ugharimu kati ya shilingi milioni 8
hadi shilingi milioni 20 kwa mtoto mmoja.
Kwa upande wake Mkuu wa
kitengo cha Vihatarishi na Uzingatiaji kutoka Benki ya Kenya Commercial (KCB)
tawi la Tanzania Angelina Semioni alisema KCB imepata fursa ya kugusa maisha ya
watoto wenye magonjwa ya moyo wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.
“Leo KCB imekabidhi
msaada wa shilingi milioni 20 kugharamia upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotoka
katika familia zisizokuwa na uwezo kwa kugharamia matibabu pamoja na
kuhakikisha watoto hao wanapata matibabu endelevu”, alisema Angelina
Angelina alisema KCB
inaungana na jamii katika kusaidia matibabu kwani wanaamini kuwa kila mtoto
anastahili fursa ya kuishi hivyo wakaona waweze kuwezesha uwezo wa kifedha
utakaowezesha kuokoa maisha.
“Kwetu sisi mchango huu
una maana kubwa kuliko thamani ya fedha tunayoitoa, kila mtoto atakayefanyiwa
upasuaji tunaamini atakuwa na mafanikio makubwa na tutaweza kupata maendeleo
endelevu kama taifa kupitia watoto hawa tunaowasidia leo”, alisema Angelina
Nao wazazi wa watoto
wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa na Taasisi hiyo wamewashukuru wadau mbalimbali
wanaoendelea kuchangia gharama za matibabu ili kuwezesha watoto wao kufanyiwa
upasuaji wa moyo.
Anna Gaspari mzazi wa
mtoto mwenye magonjwa ya moyo alisema baada ya kufika katika Taasisi hiyo na
mtoto wake kufanyiwa uchunguzi na kutakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo alipewa gharama
za shilingi milioni 10 ambazo hakuwa na uwezo wa kulipia.
“Sikuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu ili mwanangu aweze kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha valvu za moyo lakini kupitia kitengo cha ustawi wa jamii mtoto wangu amefanyiwa upasuaji wa moyo kupitia fedha zinazotolewa na wadau kusaidia upasuaji wa moyo kwa watoto”, alisema Anna



.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment