Watu 546 wapimwa Namba Zao katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Dodoma
Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyokuwa yakifanyika katika Viwanja vya Chinangali Park na kumalizika leo jijini Dodoma. Jumla ya watu 546 wamepimwa Namba Zao.
Afisa Uuguzi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bakar Mohamed akimpima shinikizo la damu
mwananchi aliyefika katika banda la Taasisi hiyo kwaajili ya kujua Namba Zake
wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyokuwa yakifanyika katika
Viwanja vya Chinangali Park na kumalizika leo jijini Dodoma. Jumla ya watu 546
wamepimwa Namba Zao.
Wananchi wakiendelea
kupata elimu kuhusu Namba Zao katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyokuwa yakifanyika
katika Viwanja vya Chinangali Park na kumalizika leo jijini Dodoma. Jumla ya
watu 546 wamepimwa Namba Zao.
Na JKCI
*************************************************************************************************
Jumla ya watu 546
wamefanyiwa uchunguzi wa afya kwa kupimwa Namba Zao wakati wa kambi maalumu ya
uchunguzi wa afya iliyokuwa ikifanyika katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Kupitia kambi hiyo iliyomalizika
leo katika Viwanja vya Chinangali Park vilivyopo jijini Dodoma watu
waliotembelea katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walifanyiwa
vipimo vya kuchunguza ugonjwa wa shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye
damu, uwiano wa urefu kwa uzito pamoja na mzunguko wa kiuno.
Aidha watu 192
walifanyiwa kipimo cha kuchunguza utendaji kazi wa moyo (Echocardiography –
ECHO), huku watu 11 wakifanyiwa kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo
(Electrocardiography – ECG).
Akizungumza wakati wa kuhitimisha
kambi hiyo Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Daud Gwilenza
alisema watu 94 wamepewa rufaa kwenda katika Taasisi hiyo kwa ajili ya
uchunguzi zaidi.
“Watu 82 tumewabaini
kuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, huku watu 20 tumewabaini kuwa na
tatizo la sukari. Baadhi ya watu hawa walikuwa tayari wanajua hali zao lakini wengine
hawakuwa wanajua kama wana matatizo ya shinikizo la damu na sukari”, alisema
Dkt. Daud.
Dkt. Daud aliongeza
kuwa magonjwa mengine yaliyobainika kupitia kambi hiyo ni pamoja na kuziba kwa
mishipa ya damu ya moyo na kutanuka kwa moyo hali ambayo kwa kiasi kikubwa
husababishwa na shinikizo la damu la muda mrefu.
“Jamii inapaswa kujenga
utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, hii itatusaidia kulinda
afya zetu na kuchukua hatua mapema tunapogundulika kuwa na magonjwa
yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yanaongezeka kwa kasi katika jamii yetu”,
alisema Dkt. Daud.
Kwa upande wao wananchi
waliopata huduma katika banda la JKCI waliishukuru Serikali kwa kuwezesha
kufanyika kwa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mkoani Dodoma jambo
lililowapa fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa afya bila gharama.
James Balilonga mkazi
wa Dodoma alisema maonesho hayo yamemsaidia kutambua umuhimu wa kufanya
uchunguzi wa afya hata pale mtu anapokuwa hana dalili za ugonjwa.
“Unapokutana na
wataalamu wa afya na kupata elimu kuhusu umuhimu wa kuchunguza afya unahamasika kuchukua hatua. Hili
limekuwa fundisho kwangu kwamba siyo lazima nisubiri kuumwa ndipo nifanye
uchunguzi wa afya”, alisema James.
Naye Doris Mwirezeyo
alizitaka taasisi za afya kuanzia ngazi ya Wilaya kuendelea kutoa elimu kwa
jamii kuhusu umuhimu wa kuchunguza afya mara kwa mara ili kuwasaidia wananchi
kujikinga na magonjwa na kupata matibabu kwa wakati.
“Leo nimejifunza jambo
muhimu, kama tungekuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara na kuzingatia
mtindo bora wa maisha pengine tusingekuwa na wagonjwa wengi wenye matatizo ya
moyo, elimu hii inapaswa kuwafikia wananchi hadi ngazi za chini ili waweze
kujilinda”, alisema Doris.
Comments
Post a Comment