UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA ZA MGONJWA ZINAZOSAMBAA MTANDAONI


Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa za mgonjwa zinazosambaa mtandaoni kuhusu matibabu aliyokuwa akipatiwa katika Taasisi yetu. 

Mgonjwa huyo alipokelewa JKCI tarehe 25 Mei 2026 akiwa na matatizo makubwa ya moyo yaliyosababisha moyo kushindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa. Mara baada ya kulazwa, alipatiwa matibabu ya kina kwa lengo la kuimarisha hali yake ili aweze kuendelea na hatua nyingine za matibabu ikiwemo upasuaji wa moyo. Katika kipindi cha matibabu jopo la wataalamu wakiwemo madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo walikutana na mgonjwa pamoja na ndugu zake kuwaeleza kwa kina hali ya mgonjwa na hatari zilizokuwepo. 

Wataalamu walieleza kuwa kufanya upasuaji katika kipindi hicho kungeweza kuhatarisha zaidi maisha yake kutokana na hali yake kuwa dhaifu hivyo ilikubaliwa aendelee na matibabu ya kuimarisha afya yake. Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na wataalamu wetu na matibabu yote aliyokuwa akipatiwa hali ya mgonjwa iliendelea kutoimarika kutokana na changamoto za kiafya alizokuwa nazo hivyo kutotakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo. 

JKCI inasisitiza kuwa mgonjwa alipatiwa huduma stahiki kwa mujibu wa miongozo ya kitaalamu na familia yake iliendelea kupewa taarifa kuhusu maendeleo ya hali yake katika kipindi chote cha matibabu. 

Taarifa zote muhimu kuhusu hali ya mgonjwa zilishirikishwa kwa ndugu wa mgonjwa kwa uwazi. Taasisi inasikitishwa na upotoshaji unaodai kuwa mgonjwa hakupatiwa huduma zinazostahili, tunaendelea kusisitiza dhamira yetu ya kutoa huduma bora za matibabu kwa weledi, uwazi na kuzingatia maadili ya taaluma ya afya. 

 “Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Letu” 

 Imetolewa na: 

 Genofeva Matemu 

 Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano 

 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete

Comments

Popular posts from this blog

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi