JKCI yashiriki mkutano wa kimataifa kujadili mikakati ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza Afrika PEN-PLUS (ICPPA 2026)
Watalaamu wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wameshiriki katika mkutano mkuu wa tatu wa Kimataifa
wa kikanda PEN-PLUS (ICPPA 2026) ili kujadili changamoto mbalimbali
zinazokwamisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na kufikia maamuzi ya
pamoja yatakayosaidia kufanikisha malengo ya afya kuelekea dira 2050.
Akizungumza wakati wa
mkutano huo Daktari Bingwa wa Upasuaji
wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Msoka alisema mkutano huo
umesaidia kuwakutanisha wadau mbalimbali
kutoka nchi za Afrika kujadili kwa
pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na magonjwa hayo.
Dkt. Msoka alisema
magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi katika Bara la Afrika jambo linalohitaji
hatua za haraka na ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuyadhibiti.
“JKCI kama mdau katika
mkutano huu tunashiriki kikamilifu katika kujadili changanmoto zilizopo na
kutafuta suluhisho zake ili kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu namna
ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwani takwimu zinaonesha kuwa asilimia
35 ya vifo nchini vinatokana na magonjwa hayo”, alisema Dkt. Msoka.
Dkt. Msoka alisema
kupitia mkutano huo JKCI imeweka banda la maonesho kuwaonesha wataalamu kutoka
nchi washiriki wa mkutano huo huduma inazozitoa na namna ambavyo imeleta
mabadiliko makubwa katika matibabu ya moyo Afrika Mashariki na Kati.
“Kumekuwa na changamoto
nyingi zinazotokana na mtindo usiofaa wa maisha katika ukanda wetu kama vile kutokufanya
mazoezi, matumizi ya pombe kupita kiasi na kutokufuata lishe bora, hizi ni
miongoni mwa sababu kuu zinazochangia magonjwa yasiyoambukiza, hivyo sisi kama
JKCI tunaendelea kupambana na magonjwa hayo katika jamii yetu”, alisema Msoka.
Baadhi ya washiriki wa
mkutano huo waliotembelea banda la JKCI walipongeza jitihada za Serikali ya
Tanzania kwa kuendelea kuboresha huduma za afya hususani huduma bingwa bobezi
za magonjwa ya moyo.
“Huduma zinazotolewa na
JKCI ni huduma za kiwango cha juu, naiomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa
wananchi wake hususani walioko vijijini ili wanapokumbana na changamoto za
magonjwa ya moyo waweze kupata huduma kwa wakati”, alisema Padri Cosmas Mgina
wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Dar es Salaam.
Kwa upande wake Daktari
kutoka nchini Ghana Wallace Ollen alisema JKCI imekuwa mfano wa kuigwa barani
Afrika kwa kutoa huduma za kibingwa bobezi za matibabu ya magonjwa ya moyo na
mishipa ya damu.
“Naipongeza JKCI kwani
upatikanaji wa huduma za matibabu ya moyo Barani Afrika umekuwa msaada mkubwa
kwa wananchi wetu kwa kuwa sasa hatuna sababu ya kusafiri kwenda mataifa
mengine kama India kupata matibabu bingwa ya moyo”, alisema Dkt. Ollen.
-Mwisho-
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment