JKCI, Israel waimarisha huduma za upasuaji wa Moyo kwa watoto 252
Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani akitoa historia
ya JKCI kwa balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Gideon Behar wakati
alipotembelea Taasisi hiyo hiyo hivi
karibuni kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo
zinazotolewa pamoja na uwekezaji mkubwa
uliofanywa na serikali ya Tanzania katika matibabu ya moyo.
Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Gideon Behar akiongea na waandishi wa habari wakati alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) hivi karibuni kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Tanzania katika matibabu ya moyo.
Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani akimkabidhi
zawadi Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Gideon Behar alipotembelea JKCI hivi karibuni kwaajili ya
kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na uwekezaji
mkubwa uliofanywa na serikali ya Tanzania katika matibabu ya moyo.
Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Moyo kwa Watoto na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akimuonesha Balozi wa Israel
nchini Tanzania Mhe. Gideon Behar baadhi
ya maeneo ya taasisi hiyo wakati alipotembelea taasisi hiyo kuona uwekezaji mkubwa
uliofanywa na serikali ya Tanzania pamoja na huduma za matibabu ya moyo
zinazotolea.
Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Moyo kwa Watoto na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akizungumza na Balozi wa Israel
nchini Tanzania Mhe. Gideon Behar kuhusu
huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo wakati balozi huyo alipotembelea taasisi
hiyo kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Tanzania katika matibabu ya
moyo.
Mkuu
wa Kitengo cha Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Thadei Kavishe
akimuelezea Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Gideon Behar huduma zinazotolewa na maabara hiyo ya kisasa inayotumia teknolojia
ya roboti kufanya vipimo mbalimbali wakati balozi huyo alipo tembelea taasisi hiyo
kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Tanzania.
Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Gideon Behar na baadhi ya Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya balozi huyo kumaliza ziara yake ya kutembelea taasisi hiyo kwaajili ya kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Tanzania katika matibabu ya moyo na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Na JKCI
***************************************************************************************************
Kati ya watoto hao 170 walifanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi
maalumu zilizofanywa hapa nchini na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na
wenzao wa SACH huku watoto 82
wakipelekwa nchini Israel kwa matibabu zaidi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa
JKCI, Dkt. Naizihijwa Majani
alipokuwa akizungumza na Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Gideon Behar alipotembelea
taasisi hiyo kujionea huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na
uwekezaji uliofanywa na serikali ya Tanzania katika
matibabu ya moyo.
Ziara hiyo ya Mhe. Balozi mpya wa Israel nchini Tanzania katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
iliyopo jijini Dar es Salaam ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano kati
ya nchi hizo mbili katika sekta ya afya.
Dkt. Naizihijwa
ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto alisema tangu kuanza kwa ushirikiano huo Israel imekuwa ikiunga mkono juhudi za JKCI
katika kuboresha huduma za moyo kwa watoto.
“Tumefanya mambo makubwa kwa pamoja ikiwemo wataalamu wetu 15
kupata mafunzo nchini Israel jambo
ambalo limesaidia kuongeza idadi ya watoto wanaopata matibabu hapa nchini na
kupunguza rufaa za kwenda kutibiwa nje
ya nchi”, alisema Dkt. Naizihijwa.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo umevuka mipaka ya Tanzania kwa
kuhusisha pia nchi jirani za Zambia, Kenya, Rwanda na Uganda jambo lililoongeza
tija katika utoaji wa huduma na kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi barani
Afrika.
Dkt. Naizihijwa
alisema kupitia ushirikiano na SACH, JKCI pia inaisimamia hospitali ya moyo ya
Zambia kwa kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto, kutoa mafunzo kwa wataalamu
pamoja na kufanya tafiti mbalimbali za afya.
Kwa upande wake Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Behar
alisema mahusiano ya muda mrefu kati ya JKCI na Israel yamekuwa na manufaa
makubwa hususan kupitia Shirika la Save
a Child’s Heart (SACH) ambalo
limechangia kuokoa maisha ya watoto wengi wenye matatizo ya moyo.
Mhe.Balozi Behar alisema mahusiano kati ya Israel na Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni mfano wa kuigwa katika ushirikiano wa kimataifa
wenye lengo la kuokoa maisha ya watu hususan watoto.
Alisisitiza kuwa ushirikiano huo umejengwa katika msingi wa
kuaminiana, kubadilishana ujuzi na teknolojia ya kisasa ya tiba ya moyo na
kwamba Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha watoto wengi
zaidi wanaozaliwa na matatizo ya moyo wanapata matibabu bora kwa wakati.
“JKCI mnafanya kazi nzuri.
Nimepita katika maeneo mbalimbali na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanyika, niko
tayari kuendeleza ushirikiano huu wa kihistoria ili kuhakikisha watoto
wanaozaliwa na matatizo ya moyo wanapatiwa matibabu kwa ufanisi. Kwa Kiyahudi
tunasema, ukiokoa maisha ya mtoto mmoja umeokoa maisha ya dunia nzima”, alisema Mhe. Balozi Behar.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Moyo kwa watoto wa JKCI
ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto Dkt. Godwin Sharau alisema ushirikiano huo
umeleta mafanikio makubwa katika tiba ya moyo kwa watoto si Tanzania pekee bali
pia katika ukanda wa Afrika.
Dkt. Godwin alisema
madaktari wengi pamoja na wauguzi wanaofanya
upasuaji wa moyo kwa watoto katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wamepata mafunzo yao nchini Israel kupitia ushirikiano na Shirika la Save a
Child’s Heart (SACH).
Alieleza kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kitaalamu na
kuwapa ujuzi wa kutumia teknolojia za kisasa pamoja na mbinu bora za matibabu
ya moyo kwa watoto jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma
zinazotolewa nchini na kuongeza uwezo wa kufanya upasuaji wenye mafanikio
makubwa hapa nyumbani.
“Ujuzi tulioupata nchini Israel umetuwezesha kutoa huduma bora
hapa nyumbani na kusaidia nchi jirani zinazoanzisha vitengo vya matibabu ya
moyo kwa watoto kufikia ufanisi wa juu. Kwa ufupi sisi ni mbegu iliyotoka
Israel na kuja kupandwa Afrika”, alisema
Dkt. Sharau.
Akiwa
katika Taasisi hiyo Mhe. Balozi Behar alitembelea maeneo mbalimbali ikiwemo
vyumba vya upasuaji, wodi za wagonjwa, kliniki za wagonjwa pamoja na maabara ya
kisasa inayotumia mfumo wa roboti kupima sampuli mbalimbali zikiwemo za damu
ambapo alijionea kwa karibu namna huduma za kibingwa na kibobezi za moyo
zinavyotolewa kwa ufanisi mkubwa na teknolojia ya kisasa.







Comments
Post a Comment