Serikali yajipanga kusogeza huduma bingwa za Moyo karibu na Wananchi
Meneja wa Rasilimali watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Hospitali ya Dar Group Abdulrahman Muya akimkabidhi Waziri wa Kazi Mhe.
Deus Clement Sanga zawadi ya mashine ya BP, RBG na Thermometer kama sehemu ya
kampeni ya kuhamasisha jamii kujua namba zao za afya alipotembelea banda la
taasisi hiyo lililopo kwenye maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi
yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema Mjini Njombe.
Daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na kazi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elius Birago akimueleza Waziri wa Kazi Mhe. Deus Clement Sanga huduma
zinazotolewa na Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa
Kazi yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema Mjini Njombe.
Daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na kazi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elius Birago akimpa zawadi
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Juma Mfanga alipotembelea banda la Taasisi
hiyo wakati wa maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika
viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema Mjini Njombe.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Happiness Shirima akitoa elimu kuhusu magonjwa ya moyo
na namna ya kujikinga na magonjwa hayo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya
Lunyanywi walipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya Usalama na
Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema
Mjini Njombe.
Picha na JKCI
*******************************************************************************************************
Serikali kupitia Wizara
ya Kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imeahidi kuweka mikakati madhubuti
ya kuiwezesha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kufikisha huduma bingwa na
bobezi za uchunguzi na matibabu ya moyo katika mikoa yote nchini hatua
inayolenga kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi.
Hayo yamesema jana na
Waziri wa Kazi Mhe. Deus Clement Sanga
alipotembelea banda la JKCI katika maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi
yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema mjini Njombe.
Akiwa katika banda hilo
Waziri Sanga alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na
wataalamu wa JKCI pamoja na mwitikio mkubwa wa wananchi waliojitokeza kupima
afya zao.
Mhe. Sanga alisema
mahitaji ya huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo yanaendelea kuongezeka
kutokana na kasi ya magonjwa yasiyoambukiza hivyo kuna umuhimu mkubwa wa
kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kwa urahisi zaidi.
“Mwitikio mkubwa wa
wananchi wa Njombe ni ishara tosha ya uhitaji wa huduma hizi za uchunguzi na
matibabu ya moyo na kuhimiza JKCI kutumia fursa hiyo kufanya tathmini ya kina
itakayosaidia kupanga mikakati ya kufikisha huduma hizo kwa upana zaidi”.
“Kaulimbiu ya mwaka huu
inayozungumzia umuhimu wa mazingira bora ya kisaikolojia mahali pa kazi ina
uhusiano wa moja kwa moja na afya ya moyo, kwani msongo wa mawazo unaweza
kuchangia ongezeko la magonjwa ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo”,
alisema Mhe. Sanga.
Waziri huyo wa Kazi
aliwapongezata wataalamu wa JKCI kwa kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na
magonjwa ya moyo katika maonesho hayo huku akisema imewasaidia wafanyakazi na
wananchi kuelewa namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kupitia
mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Kwa upande wake Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka JKCI, Moses Manumbu alisema mwitikio wa
wananchi wa Njombe umekuwa mkubwa na wenye hamasa ya kujua hali zao za afya.
Dkt. Manumbu alieleza
kuwa watu wengi wamejitokeza kupima moyo na kupata ushauri wa kitaalamu huku wengi wao wakiomba huduma hizo ziendelee
kutolewa hata baada ya maonesho hayo kukamilika.
“Tumebaini kuwa kuna
watu wengi wanaishi na magonjwa yasiyoambukiza bila ya wao kufahamu hali inayoonyesha umuhimu wa uchunguzi wa
mara kwa mara. Wananchi wameonesha uhitaji mkubwa wa huduma hizi kuendelea
kufikishwa hapa Njombe angalau mara moja au mbili kwa mwaka”, alisema Dkt. Manumbu.
Naye Paulo Mbando mkazi
wa Njombe alisema amenufaika na huduma hizo kwa kupima afya ya moyo bure pamoja
na kupata elimu ya mtindo bora wa maisha kutoka kwa wataalamu wa JKCI, huduma
hizo ni matokeo ya juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma
za afya na kuwajali wananchi wake.
“Leo nimepata fursa ya
kupima moyo bila gharama na kupewa elimu muhimu itakayosaidia kulinda afya
yangu. Hii ni hatua kubwa kwetu wananchi, naamini kupitia elimu hii nitaweza
kujilinda nisipate magonjwa ya moyo”, alisema Paulo.
Comments
Post a Comment