Ushirikiano wataalamu wa JKCI na China kuokoa maisha na kupunguza rufaa za wagonjwa wa moyo kwenda nje ya nchi

Mkurugenzi wa upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwaaaga madaktari bingwa wa moyo kutoka Jamhuri ya Watu wa China waliokuwa wakifanya kazi katika Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. Hafla hiyo imefanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akimkabidhi zawadi daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Jamhuri ya watu wa China Zhao Lijian wakati wa hafla fupi ya kuwaaaga madaktari kutoka China iliyofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akimkabidhi cheti daktari bingwa wa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu kutoka Jamhuri ya watu wa China Zhang Mingming wakati wa hafla fupi ya kuwaaaga madaktari kutoka wa China iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akimkabidhi tuzo ya shukrani daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Jamhuri ya watu wa China Liu YiMin wakati wa hafla fupi ya kuwaaaga madaktari kutoka China iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Edna Kajuna akitoa neno la shukrani kwa madaktari kutoka Jamhuri ya watu wa China waliofanya kazi katika Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili wakati wa hafla fupi ya kuwaaaga madaktari hao iliyofanyika leo katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja na madakatri kutoka Jamhuri ya Watu wa China mara baada ya hafla fupi ya kuwaaga madakatri hao iliyofanyika leo katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Na JKCI
**************************************************************************************************************

Ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya afya kati Tanzania na China umeongeza mafanikio katika kutoa huduma bingwa bobezi za upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wa moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Hatua hiyo imechangia kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wenye matatizo ya moyo na kupunguza rufaa za wagonjwa wa moyo kwenda nje ya nchi kwaajili ya matibabu.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwaaga madaktari bingwa wa moyo kutoka nchini China kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili na kuleta watalaamu wa afya kutoka China kubadilishana ujuzi na wataalamu wa nchini Tanzania.

“Kundi la 27 la madaktari bingwa bobezi wa moyo limeleta mafanikio makubwa katika kutoa huduma bingwa bobezi za moyo kwani kabla ya ujio wao kuna baadhi ya upasuaji wa moyo kwa watoto kwa kutumia tundu dogo ulikuwa haufanyika hapa nchini lakini kupitia wao tumeweza kufanya upasuaji huo, kupunguza maumivu kwa wagonjwa na kuwawezesha kupona haraka”,

“Hadi sasa JKCI imezalisha wataalamu watatu ambao wanafanya upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo kwa watoto kupita ujuzi walioupata kwa wataalamu kutoka China, tutaendelea kushirikiana nao kwa karibu lengo likiwa kuwasaidia wagonjwa wetu”, alisema Dkt. Angela

Kwa Upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka JKCI Evarist Nyawawa alisema watalaamu kutoka China wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kurahisisha utoaji wa huduma.

Kupitia kundi la 27 la wataalamu kutoka China wataalamu wa JKCI wanaofanya kazi katika idara ya upasuaji wa moyo, idara ya magonjwa ya moyo kwa watoto na chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) wameweza kubadilishana ujuzi na wengine kupata fursa ya kwenda nchini China kuongeza ujuzi.

 “Tumefaidika sana kwa uwepo wa wataalamu hawa kutoka China kwani wamehudumia wagonjwa wetu kwa bidii, weledi na kujituma hali iliyosaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa”, alisema Dkt. Nyawawa.

Naye Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Hospitali ya Shandong iliyopo nchini China Liu YiMin alisema ushirikiano baina ya Tanzania na China umemwezesha kutoa mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya wagonjwa wa moyo waliopo nchini Tanzania.

“Katika kipindi cha miaka miwili tuliyokaa Tanzania nimejifunza mambo mengi kutoka kwa wataalamu wenzetu, pia nimeona jinsi ambavyo Serikali ya Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba vya moyo ambao unaifanya Taasisi hii kuwa bora Afrika Mashariki na Kati katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo”, alisema Liu.

Akitoa neno la Shukrani Afisa Uuguzi kutoka JKCI Edna Kajuna alisema ujio wa wataalamu hao umeongeza uwezo wa taasisi katika kuwahudumia wagonjwa wengi kwa kipindi cha muda mfupi.

“Kundi la 27 la wataalamu kutoka nchini China limetusaidia hivyo kutoa huduma za upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo kwa watoto hadi 30 kwa mwezi, hii ni hatua kubwa katika kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo nchini”, alisema Edna.

Comments