JKCI yawajengea uwezo viongozi katika usimamizi wa vihatarishi kwaajili ya ufanisi wa malengo

 

Menejimenti ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  inahudhuria mafunzo maalumu ya siku mbili yanayolenga  kuwajengea uwezo wa kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kujitokeza na kuathiri taasisi hiyo katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa wanaowahudumia.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge  wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Kitengo cha Sheria Adv.  Maulid Kikondo alisema ni takwa la kisheria kwa taasisi za umma na binafsi kuwajengea uwezo viongozi wake ili waweze kutambua na kudhibiti hatari katika maeneo yao ya kazi sambamba na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Adv. Kikondo alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa viongozi katika kulinda taasisi dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kujitokeza ili waweze kufahamu mbinu bora za kukabiliana navyo na kuepusha usumbufu au kusitishwa kwa huduma za afya kwa wananchi.

“Taasisi inapokuwa na viongozi wenye uelewa wa kutosha kuhusu usimamizi wa hatari inakuwa rahisi kupanga mikakati ya mapema ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza na hivyo kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa bila vikwazo”, alisema Adv. Kikondo.

Adv. Kikondo aliongeza kuwa mafunzo hayo yataisaidia JKCI kuendelea kuwa taasisi imara na yenye uwezo wa kujibu changamoto mbalimbali kwa wakati huku ikiweka mbele usalama wa wagonjwa, watumishi na rasilimali za taasisi.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu  Mzumbe Kampasi Kuu ya Morogoro Dkt. Cosmos Mbogela alisema vihatarishi hutokea wakati wa utekelezaji wa mipango na vinaweza kusababisha taasisi kushindwa kufikia malengo yake na hatimaye kuleta madhara.

“Mafunzo haya ni muhimu kuhuishwa kila mwaka kwani vihatarishi vina tabia ya kubadilika. Hivyo ni muhimu kuweka mikakati ya kuhakikisha hatari haitokei na endapo itatokea idhibitiwe mapema”,  alisema Dkt. Mbogela.

Dkt. Mbogela alisema  taasisi nyingi hukumbwa na changamoto kubwa pale zinaposhindwa kutambua vihatarishi mapema jambo ambalo huweza kuathiri utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku pamoja na kushusha kiwango cha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alisisitiza kuwa usimamizi bora wa vihatarishi unahitaji ushirikiano wa viongozi na watumishi wote ndani ya taasisi kwani kila mmoja ana wajibu wa kubaini mapema viashiria vya hatari na kuchukua hatua stahiki kabla madhara hayajatokea.

Nao viongozi walioshiriki katika mafunzo hayo walisema yamekuwa yenye manufaa makubwa kwao kwani yamewapa uelewa mpana kuhusu namna ya kutambua vihatarishi katika maeneo yao ya kazi na kuweka mikakati madhubuti ya kuvizuia au kuvipunguza kabla havijaleta madhara.

“Mafunzo haya yatatusaidia viongozi kubaini vihatarishi na kuweka mikakati ya kukabiliana navyo ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaofika katika taasisi yetu kupata huduma”.

“Hii ni fursa kwetu viongozi kuboresha maeneo yetu ya kazi kwa manufaa ya wananchi na watu tunaowaongoza kwani ikiwa hatari itatokea na tukashindwa kuidhibiti mapema wagonjwa wanaweza kupata madhara”, alisema Robet Mallya Mkurugenzi wa Uuguzi.

Akielezea umuhimu wa mafunzo hayo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Renatha Miiruko alisema ikiwa vihatarishi havitawekewa mikakati ya kudhibitiwa vinaweza kusababisha hasara katika utendaji wa taasisi.

“Vihatarishi vinaweza kuipeleka taasisi katika hali isiyotarajiwa iwapo havitachukuliwa hatua stahiki. Hivyo ni muhimu kufanyia kazi mafunzo haya ili kusaidia kuilinda taasisi dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kuchelewa kuchukua hatua” alisema Renatha.

CPA. Juma Mshana ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa ndani alisema mafunzo hayo ni msaada mkubwa kwa viongozi hao  kwani yameongeza uelewa wa namna ya kutambua maeneo yenye hatari  kiutendaji na kiutawala ndani ya taasisi uelewa huo utasaidia kuimarisha udhibiti wa ndani na kuhakikisha rasilimali za taasisi zinatumika kwa ufanisi na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

“Kitengo cha Ukaguzi wa ndani kina nafasi muhimu katika kuzuia na kugundua mapema vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji wa taasisi. Kupitia mafunzo haya tutaweza kuboresha mbinu za ukaguzi na kufanya kazi kwa karibu zaidi na menejimenti katika kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na usalama wa rasilimali za taasisi vinaimarika kwa manufaa ya utoaji bora wa huduma za afya”, alisema CPA. Mshana.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi