Jamii yahimizwa kutambua vihatarishi vya magonjwa ya moyo mapema
Mhudumu wa Afya wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Halima Shaban akimpima uwiano wa urefu na
uzito mwananchi aliyejitokeza kufanya uchunguzi wa afya wakati wa kambi maalumu
ya siku tatu ya uchunguzi wa afya inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo katika kliniki
ya JKCI iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Na JKCI
************************************************************************************************
Jamii imetakiwa
kuendelea kuhamasika kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kufahamu
vihatarishi vinavyoweza kuhatarisha afya zao na kusababisha magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
Rai hiyo imetolewa leo na
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Rafael Kwileka wakati wa kambi
maalumu ya siku tatu ya uchunguzi wa afya inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo katika
kliniki ya JKCI iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Rafael alisema
kupitia kambi hiyo wananchi waliojitokeza wameweza kupata elimu ya mtindo bora
wa maisha, kuzingatia lishe bora na namna bora ya kuweza kujikinga na magonjwa
ya moyo ili kupunguza gharama zinazotumika kuyatibu magonjwa hayo.
“JKCI sasa tuna
kaulimbiu yetu ya jua namba zao za afya ambayo tumeitumia katika kambi hii
kuihamasisha jamii kufanya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya shinikizo la damu,
sukari kwenye damu, mafuta kwenye damu ambavyo vote hivi vinaweza kusababisha
magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Rafael
Dkt. Rafael alisema
wamefurahi kuona kupitia kambi hiyo watu wenye umri wa miaka 40 na kuendelea
wamejitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa afya kwani watu wenye umri huo ni
muhimu kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara.
Aidha Dkt. Rafael
alisema kupitia kambi hiyo JKCI kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Damu Salama
wameendesha zoezi la uchangiaji wa damu zitakazoenda kutumika kwa wagonjwa
wanaofanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi hiyo.
Kwa upande wake
mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Venance Mushi aliipongeza JKCI
kwa kusogeza huduma karibu kwa wafanyabiasha wa Kariakoo kwani zinawahamasisha
kufanya uchunguzi wa afya na hata pale wanapotaka kujisahau kufuatilia afya zao
wanakumbuka kuwa afya ni muhimu kuliko vyote.
“Nawashauri watu wapime
afya zao hata mara moja kwa mwaka kwani hakuna kitu kizuri kama kuishi huku
unajitambua, tumekuwa bize kuliko afya zetu ndio maana kuna wakati unakuta watu
wanaanguka ghafla na wanaowazunguka wanashindwa kujua waanzie wapi”, alisema
Mushi
Mushi alisema
alitembekea kambi hiyo kwa lengo la kuchangia damu kama ambavyo imekuwa kawaida
yake kuchangia damu kila mwaka lakini alivofika katika kambi hiyo akahamasika kufanya
uchunguzi wa afya.
“Naipenda sana afya
yangu na uwepo wa Taasisi hii katika Soko la Kariakoo imekuwa fursa kwangu
kufanya uchunguzi wa afya”, alisema Mushi.
Naye Veronica Innocent
mkazi wa Ilala alisema kama kijana amehamasika kufanya uchunguzi wa afya mara
baada ya kukutana na kambi hivyo kuwataka vijana wanapokutana na fursa kama
hizo wazitumie kuchunguza afya zao.
“Namshukuru Mungu baada
ya kufanya uchunguzi wa afya nimekutwa salama na kupewa elimu ya namna naweza
kujikinga na magonjwa ya moyo, kuanzia leo nitaishi kwa kufuata elimu
niliyoipata hapa”, alisema Veronica



Comments
Post a Comment