Msaada wa Rais Samia wamfungulia milango ya matibabu: Mtoto mwenye tatizo la Moyo aanza safari JKCI
Mtoto Selina Daudi anayekabiliwa na changamoto ya tundu kwenye moyo ameanza rasmi safari ya matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kufuatia kupatiwa msaada wa kifedha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Selina anayeishi na mama yake Aisha Said
katika eneo la Chanika jijini Dar es Salaam anatarajiwa kupata huduma za
kibingwa zitakazomsaidia kurejea katika hali yake ya kawaida kiafya.
Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa
JKCI, Peter Kisenge alisema msaada uliotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia umefungua
ukurasa mpya wa matumaini kwa mtoto huyo huku gharama za matibabu zikifikia
zaidi ya shilingi milioni nane.
Mbali na msaada huo Dkt. Kisenge alieleza
kuguswa na hali ya mtoto huyo na kuamua kujitolea kugharamia masomo yake yote
huku akiahidi kulipia ada ya shule kupitia kipato chake binafsi.
Kwa upande wa huduma za kitabibu Daktari
bingwa wa watoto wa JKCI, Sulende Kubhoja alibainisha kuwa maendeleo ya sayansi
na teknolojia yameongeza uwezo wa wataalamu kugundua mapema matatizo ya moyo
kwa watoto na kutoa tiba stahiki kwa wakati.
Aliongeza kuwa kila siku taasisi hiyo hupokea
watoto wengi wenye matatizo ya moyo ambapo wastani wa wagonjwa 50 wanaopekelewa
kati yao takribani 20 huhitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Naye mama wa mtoto huyo Aisha Said alishukuru
kwa msaada alioupata na kusema kuwa umempa faraja kubwa na moyo wa matumaini kwake
na familia yake.
“Kwa kweli nina shukrani nyingi kwa Mhe. Rais Dkt.
Samia kwa msaada huu. Naamini mwanangu atapata matibabu na kupona na kuendelea
na maisha kama watoto wengine ambao hawana matatizo ya moyo”, alisema Aisha.
Hatua hiyo inaendelea kuonesha juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha wananchi hususan wenye mahitaji ya matibabu ya kibingwa wanapata huduma muhimu kwa wakati.

Comments
Post a Comment