Mapinduzi sekta ya Afya: JKCI yaleta teknolojia ya Roboti ya bilioni 5.5

Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mariam Steven akiangalia hatua za upimaji wa sampuli za damu zinavyofanyika katika maabara ya kisasa ya taasisi hiyo inayotumia teknolojia ya roboti.


 Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Glory Mtui akiiruhusu roboti kuendelea na upimaji wa sampuli za damu kwa kutumia teknolojia ya roboti inayotumika katika maabara ya kisasa ya taasisi hiyo.


 Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Glory Mtui akipanga sampuli za damu tayari kwa upimaji kwa kutumia teknolojia ya roboti inayotumika katika maabara ya kisasa ya taasisi hiyo.

************************************************************************************************************************************************************************************************************************

Sekta ya afya nchini imepiga hatua kubwa kufuatia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuanza kutumia maabara ya kisasa yenye teknolojia ya roboti ya thamani ya shilingi bilioni 5.5 inayotarajiwa kuleta mapinduzi katika upimaji wa magonjwa mbalimbali  hususan ya moyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema maabara hiyo ni miongoni mwa maabara kubwa na za kisasa zaidi katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwa na uwezo wa kupima sampuli kwa haraka na usahihi wa hali ya juu kwa wagonjwa wa ndani na nje ya taasisi hiyo.

Alisema uwekezaji huo mkubwa wa Serikali umeongeza ufanisi wa huduma huku ukipunguza kwa kiasi kikubwa makosa ya kibinadamu katika uchunguzi wa maabara.

“Maabara hii ina mifumo ya kisasa yenye uwezo wa kutambua magonjwa hata katika hatua za awali kabisa. Pia imepunguza muda wa kusubiri majibu ya vipimo kutoka saa tatu hadi saa moja tu”, alisema Dkt. Kisenge.

Aliongeza kuwa teknolojia hiyo ina uwezo wa kuchakata idadi kubwa ya sampuli kwa muda mfupi, hatua inayochangia kupunguza muda wa mgonjwa kukaa hospitalini ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi zaidi.

Mbali na utoaji wa huduma, Dkt. Kisenge alisema maabara hiyo pia inatumika kama darasa hai kwa wataalamu wa afya nchini kwaajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu.

Katika hatua nyingine, Dkt.Kisenge alibainisha kuwa JKCI inaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia ya akiliunde (Artificial Intelligence) ambapo mwaka 2024 walizindua mfumo wa kisasa unaowezesha kufuatilia hali ya mgonjwa akiwa nyumbani kwa kutumia kifaa maalumu cha Dozee.

Alifafanua kuwa teknolojia hiyo hutumia shuka maalumu ambalo huwekwa chini ya godoro la mgonjwa na kumwezesha daktari kufuatilia viashiria muhimu vya afya ikiwemo mapigo ya moyo, upumuaji na presha bila mgonjwa kufika hospitali.

“Tangu kuanzishwa kwa huduma hii wagonjwa zaidi ya 100 wamenufaika. Tunatarajia kupanua zaidi matumizi ya teknolojia hii ili kuwafikia watanzania wengi zaidi hasa walioko mbali na vituo vya huduma za afya”, alisisitiza Dkt. Kisenge.

Mkurugenzi huyo alisema JKCI imeanzisha mfumo wa kisasa wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao (online booking) ambayo ilianza kutumika mwaka 2025, ambao hadi sasa imeshahudumia wagonjwa zaidi ya 71,506. Mfumo huo unawawezesha wagonjwa kuchagua muda wa kuonana na daktari na hivyo kupunguza msongamano na muda wa kusubiri huduma.

Taasisi hiyo pia imeanzisha mfumo wa usajili wa ndugu wanaotembelea wagonjwa waliolazwa (visitors management system), unaolenga kuimarisha usalama na uratibu wa huduma wodini.

Dkt. Kisenge alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, JKCI inalenga kuboresha zaidi huduma za tiba mtandao (telecardiology) ili kupanua wigo wa huduma za kibingwa katika hospitali za kanda na mikoa nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Maabara wa JKCI Thadei Kavishe alisema maabara hiyo ina uwezo wa kupima zaidi ya sampuli 5,000 kwa saa moja.

“Tunapima aina mbalimbali za sampuli ikiwemo damu, mkojo na majimaji kutoka sehemu mbalimbali za mwili kama moyo, mapafu na tumbo”,  alisema Kavishe.

Aliwataka wadau wa sekta ya afya zikiwemo hospitali nyingine kutumia huduma za maabara hiyo kwa kuleta sampuli zao kwa uchunguzi wa uhakika na wa kisasa.

Baadhi ya wagonjwa wanaopata huduma katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wameelezea kuridhishwa na maboresho ya huduma yanayotokana na matumizi ya teknolojia ya kisasa hususan maabara ya roboti na mifumo ya tiba mtandao.

 “Zamani nilikuwa nasubiri majibu kwa muda mrefu, lakini sasa ndani ya saa moja tayari unapata majibu. Inasaidia sana kupunguza wasiwasi na kuanza matibabu mapema, huduma ya maabara imekuwa ya haraka na yenye uhakika zaidi kuliko ilivyokuwa awali”, alisema Mama Asha Mussa mkazi wa Dar es Salaam.

“Maabara ya kisasa imeongeza imani kwa wagonjwa kuhusu ubora wa huduma tunazozipata, unajisikia uko salama zaidi unapojua vipimo vinafanywa kwa teknolojia ya kisasa na kwa usahihi mkubwa. Hii inaleta matumaini makubwa kwa sisi wagonjwa wa moyo”, alisisitiza Mzee Abdallah Said mkazi wa Pwani.

Naye Neema Joseph mkazi wa Dodoma alieleza kufurahishwa na mfumo wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao huku akisema umepunguza muda wa kusubiri huduma hospitalini.

“Ninaweka miadi nikiwa nyumbani, nikifika hospitali napata huduma kwa wakati niliopanga. Hakuna tena kukaa foleni muda mrefu”, alisema Neema.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi