Huduma za kibingwa za Moyo zawafikia wakazi wa Njombe
Daktari
bingwa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moses Manumbu akimsikiliza
mwananchi aliyefika katika banda la JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya
magonjwa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo katika maonesho ya Usalama
na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mji
Mwema vilivyopo mjini Njombe.
Wananchi
wakipata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali katika banda la
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group wakati wa maonesho
ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya
Msingi Mji Mwema vilivyopo mjini Njombe.
Na JKCI
*******************************************************************************************************
Wakazi wa Mkoa wa Njombe na mikoa jirani wametakiwa
kujitokeza kwa wingi kupima afya zao zikiwemo za moyo, huduma inayotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group ili kujua hali ya afya zao na kupata elimu ya kujikinga
na magonjwa yasiyoambukiza.
Huduma hizo zinatolewa katika Maonesho ya
Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi
Mji Mwema vilivyopo mjini Njombe.
Akizungumza jana na wananchi waliofika kupata
huduma hizo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Juma Mfanga alisema kambi hiyo
itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa huo kwani ni mara ya kwanza huduma
maalumu za moyo kutolewa na wataalamu wa JKCI kupitia maonesho hayo katika mkoa
huo.
“Tumefurahi kuona kupitia maonesho haya JKCI
mmeleta kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali mkoani Njombe. Ni
muhimu wananchi wa mkoa huu wakatumia
fursa hii kujua namba zao za afya na kupata elimu ya namna ya kujikinga na
magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Dkt. Mfanga.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Njombe utaendelea
kushirikiana na JKCI kuhakikisha huduma za kibingwa za moyo zinawafikia
wananchi wengi zaidi na kupunguza adha ya kusafiri nje ya mkoa huo kutafuta
huduma hizo.
Kwa upande wake Daktari kutoka JKCI Hospitali
ya Dar Group Elius Birago alisema huduma
za uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali ikiwemo moyo ni huduma
ambazo zinatolewa na taasisi hiyo katika maonesho hayo na kuwahimiza wakazi wa Njombe kutumia fursa hiyo kujua
namba zao za afya.
Dkt. Birago alisema ni muhimu kwa jamii
kufahamu hali zao za kiafya na kuchukua hatua mapema za kujikinga na magonjwa
ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa
kasi na kuathili nguvu kazi ya taifa.
“Kutokana na ongezeko la watu
wanaopata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo, JKCI tumekuja na kampeni ya
Jua Namba Zako za Afya ili kuihamasisha jamii kujua shinikizo la damu,
kiwango cha sukari kwenye damu, uwiano wa urefu na uzito, mapigo ya moyo pamoja na mafuta mwilini”, alisema Dkt. Birago.
Dkt. Birango alisema jamii ikifahamu viashiria
hivyo mapema na kuchukua hatua stahiki itaweza kujikinga na magonjwa hayo na
kuishi maisha yenye afya bora.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
imeendelea kuweka kambi maalumu za uchunguzi wa afya katika maeneo mbalimbali
nchini ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha jamii kupima afya zao ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa
ya moyo.
Comments
Post a Comment