Dkt. Kisenge: Waandishi wa habari tumieni kalamu zenu kuhamasisha jamii kujua namba zao za afya
Baadhi ya waandishi wa
habari wakifuatilia hotuba iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa mkutano na
waandishi hao uliofanyika leo katika Ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO ulipo
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Jijini Dodoma.
Na JKCI
***************************************************************************************************
Waandishi wa habari
nchini wametakiwa kutumia kalamu zao na kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kuihamasisha jamii kujua namba zao za afya ili iweze kujikinga
na magonjwa yasiyoambukiza kujenga taifa imara na lenye afya bora.
Rai hiyo imetolewa na
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelezea miradi ya maendeleo
inayofanywa na taasisi hiyo leo katika ukumbi wa idara ya Habari Maelezo uliopo
jijini Dodoma.
Dkt. Kisenge alisema JKCI
inafanya kampeni ya “Jua Namba Zako” kuwataka
wananchi kujua shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, urefu, uzito,
mafuta mwilini, mapigo ya moyo, na utendaji kazi wa moyo lengo likiwa kupunguza
idadi ya watu wanaopata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Kampeni zote
zinazofanywa na JKCI ikiwemo hii ya jua namba zako na ile ya kuwafuata wananchi
mahali walipo kuwafanyia uchunguzi wa afya zinatokana na uwekezaji mkubwa
uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
hususan katika kuboresha afya za wananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma bingwa
bobezi za moyo”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema
magonjwa ya moyo yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo duniani yakisababisha
takribani vifo milioni 17.9 kila mwaka kulingana na takwimu za Shirika la Afya
Duniani, huku asilimia kubwa ya vifo hivyo ikitokea katika nchi zenye kipato
cha chini na cha kati ikiwemo Tanzania.
“Katika bara la Afrika ni
nchi chache tu zimefanikiwa kuwa na hospitali maalum za matibabu ya moyo
kutokana na gharama kubwa za uwekezaji zinazohitajika. Hata hivyo Tanzania
imefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi hizo huku JKCI ikitajwa kuwa kinara wa
huduma za moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la
Sahara”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema
JKCI kwa sasa inafanya upasuaji wa moyo kwa zaidi ya wagonjwa 3,000 wa moyo kwa
njia ya tundu dogo kwa mwaka, ikiwa ni idadi kubwa ikilinganishwa na taasisi
nyingine za ukanda wa Africa. Aidha taasisi
hiyo inafanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa zaidi ya wagonjwa wa moyo 800 kwa mwaka.
Mbali na upasuaji Dkt.
Kisenge alisema JKCI imefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa
kuanzisha matawi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Arusha
na Chato hatua inayosaidia kupunguza msongamano na kuongeza upatikanaji wa
huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wakati.
Katika kuimarisha
huduma Dkt. Kisenge alisema taasisi hiyo imewekeza katika matumizi ya
teknolojia za kisasa ikiwemo mfumo wa ufuatiliaji wa wagonjwa kwa kutumia akili
bandia (AI) pamoja na huduma za kuweka miadi mtandaoni hatua iliyopunguza muda
wa kusubiri huduma hospitalini na kuongeza ufanisi.
“Tumeanzisha mchakato
wa huduma za upandikizaji wa moyo nchini ambapo maandalizi yanaendelea ikiwa ni
pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wetu kwa kuwapeleka katika hospitali za
kimataifa kwaajili ya mafunzo maalum”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge
alisema katika jitihada za kupanua huduma kimataifa JKCI imekuwa ikihudumia
wagonjwa kutoka nchi mbalimbali ndani na nje ya Afrika hali inayochangia
kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa matibabu ya moyo na kuongeza
mchango katika uchumi wa taifa.
“Kwa mwaka 2025 pekee
JKCI ilitoa huduma kwa zaidi ya wagonjwa 252,000 na kuendelea kutoa huduma za
tiba mkoba katika mikoa 26 na zaidi ya wilaya 10 nchini ili kuwafikia wananchi
wengi zaidi hususan walioko maeneo ya mbali na huduma bingwa bobezi za moyo.



Comments
Post a Comment