Watoto 39 wafanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na mwenzao kutoka nchini Cameron kupitia Shirika la Mending Kids la nchini Marekani wakimalizia kumfunga kifua mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano iliyomalizaka jana katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Jumla ya watoto 39 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na upasuaji wa tundu dogo.
Na: JKCI
***************************************************************************************************************************
Watoto 39 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa
upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano
iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.
Upasuaji huo umefanywa kwa watoto waliokuwa na magonjwa
mbalimbali ya moyo ikiwemo mishipa mikubwa ya moyo kutoka sehemu isiyo sahihi, matatizo
ya mishipa ya moyo ya upande wa kushoto na kulia, na matundu kwenye moyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mkurugenzi wa upasuaji
wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi
hiyo maalumu ilikuwa ikifanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids International
la nchini Marekani.
“Watoto 22 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na
watoto 17 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa
Cathlab, pia tumeweza kudumisha mahusiano na kuzidisha ujuzi katika kutoa
huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema kupitia ujuzi wanaoupata kutoka kwa
wataalamu wengine ikiwemo Shirika la Mending Kids International wameweza
kufanya upasuaji wa moyo na kuvuka mipaka ya Tanzania ambapo sasa wanatoa
huduma katika nchi za Cameron, Morocco, Zambia na nchi nyingine lengo likiwa
kujengeana uwezo na wataalamu wengine ili kwa pamoja waweze kuokoa maisha ya
watoto wenye magonjwa ya moyo.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto
kutoka nchini Marekani Sasha Agati alisema Mending Kids International imekuwa
ikishirikiana na JKCI zaidi ya miaka 10, ambapo sasa mafanikio yamekuwa makubwa
hivyo kuifanya taasisi hiyo kuwa bora barani Afrika.
Ushirikiano wetu mzuri umesaidia kuwaleta wagonjwa kutoka
nchini Cameron kuja kufanyiwa upasuaji wa moyo hapa JKCI, ambao baada ya kufika
wamefurahia kuona kuna nchi ipo Afrika na ina ujuzi mkubwa wa kufanya upasuaji
wa moyo”, alisema Dkt. Sasha
Naye Daktari bingwa wa Upasuaji wa moyo kwa watoto kwa
kutumia mtambo wa Cathlab wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Deogratius
Nkya alisema kupitia kambi hiyo wataalamu wanaofanya upasuaji wa tundu dogo
wameweza kuwafanyia upasuaji wa moyo bila kufungua kifua watoto 16 waliokuwa na
matatizo ya moyo ya mishipa ya damu kuziba pamoja na matundu kwenye moyo.
Dkt. Nkya alisema watoto waliofanyiwa upasuaji katika kambi
hiyo wapo ambao tayari wamesharuhusiwa na wengine wanaoendelea kupata matibabu wanendelea
vizuri.
“Ni imani yetu kuwa wataalamu hawa wa Mending Kids International
wataendelea kushirikiana nasi katika kutoa matibabu ya hali ya juu na kuboresha
afya za watoto watanzania na wa Afrika.
Comments
Post a Comment