GSM Foundation na Yanga wachangia milioni 50 za matibabu ya moyo kwa watoto
Rais wa klabu ya mpira ya Yanga Eng. Hersi Said akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge mfano wa hundi ya shilingi milioni 50 fedha zilizotolewa na GSM Foundation na klabu hiyo kwa ajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi wanaotibiwa katika taasisi hiyo.
Rais wa klabu ya mpira ya Yanga Eng. Hersi Said akimjulia hali mtoto aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea taasisi hiyo leo kwa ajili ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 50 fedha zilizotolewa na GSM Foundation na klabu hiyo kwa ajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi wanaotibiwa katika taasisi hiyo.
******************************************************************************************************************************************************************************************************************
GSM Foundation na Klabu ya mpira ya Yanga wamechangia kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotoka kwenye familia zenye uwezo mdogo kiuchumi wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akikabidhi hundi ya fedha hizo leo Jijini Dar es Salaam Rais
wa klabu ya mpira ya Yanga Eng. Hersi Said
alisema mchango huo walioutoa ni sehemu ya kufungua milango kuihamasisha jamii
kuona umuhimu wa kuwasaidia watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo kwani
walichotoa hakikidhi hitaji lililopo.
Eng. Hersi alisema gharama ya upasuaji wa moyo kwa mtu mmoja ni
shilingi milioni nane, milioni 50 waliyoitoa inakwenda kutibu watoto wachache ukilinganisha
na idadi ya watoto wanaohitaji huduma hizo, GSM Foundation na klabu ya mpira ya Yanga wameona wasikae kimya kwani wakikaa
kimya hawataweza kusaidia jamii.
“Ninatoa wito kwa jamii, taasisi, vilabu vya mpira na
makampuni mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuokoa maisha ya watoto na watanzania
wenzao wanaopitia tatizo hili la magonjwa ya moyo kwa kuwasaidia kuilipia
gharama za matibabu kwa wale wasio na uwezo wa kulipa”.
“Tumeambiwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa
asilimia 70 katika matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo na inabaki
asilimia 30, hii asilimia 30 tunatakiwa kuilipa sisi watanzania na ikiwezekana
kutoa hata zaidi ya hiyo asilimia 30 ili tuweze kumpunguzia Mhe. Rais majukumu
ambayo hata sisi tunaweza kuyafanya”, alisema Eng. Hersi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI inafarijika kuona GSM Foundation
pamoja na klabu ya mpira ya Yanga wanavyojitoa
kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo.
Dkt. Kisenge alisema Taasisi hizo mbili zimeonesha kuwa
michezo si tu burudani bali pia ni jukwaa la kugusa maisha ya watanzania
kupitia msaada ambao wameutoa kwa kusaidia watoto takribani 13 kunufaika na
huduma za upasuaji wa moyo bila kugharamia malipo.
“Ninaishukuru sana GSM Foundation na klabu
ya mpira ya Yanga kwa moyo wao wa kujitoa, kwani kila mchango unaotolewa
unasaidia kupunguza orodha ya watoto wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo”,
alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema klabu ya mpira
ya Yanga imekuwa mstari wa mbele kuielimisha jamii kuhusu magonjwa ya
moyo, lakini pia kupitia Yanga na GSM Foundation wameweza kwa pamoja kubeba kwa
uzito tatizo la magonjwa ya moyo kwa watoto na kuhakikisha kuwa wanapata nafasi
ya kuishi maisha ya kawaida.
Naye mzazi wa mtoto anayetibiwa katika Taasisi hiyo Mwajuma
Shauri aliushukuru uongozi wa GSM Foundation pamoja na klabu
ya mpira ya Yanga kwa kufanikisha matibabu ya mtoto wake kwani bila
kupata msaada familia yake isingeweza kugharamia matibabu hayo.
“Gharama za matibabu ya mtoto wangu zilikuwa shilingi milioni
9 na laki 9 ambazo kwakweli kwa hali ya kawaida sikutegemea kama mwanangu
angeweza kufanyiwa upasuaji lakini kupitia kwa wadau hawa amepata matibabu”, alishukuru
Mwajuma.
Tarehe 29 Oktoba mwaka 2025 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Klabu ya mpira ya Yanga zilisaini hati ya mkataba wa ushirikiano katika utendaji wa kazi na kuielimisha jamii kuhusu magonjwa moyo.
Comments
Post a Comment