Upimaji wa moyo wafanyika katika maonesho ya Afya Zanzibar
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eva Wakuganda akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) mtoto aliyefika katika banda la Taasisi hiyo kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya wiki ya Afya Zanzibar yanayofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip Airport.
Mratibu wa utalii matibabu kutoka Wizara ya Afya Dkt. Asha
Mahita akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) alipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya wiki
ya Afya Zanzibar yanayofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip
Airport.
Na: JKCI
****************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inashiriki katika
maonesho ya wiki ya afya Zanzibar kwa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya
moyo kwa wananchi bila gharama.
Maonesho hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza Zanzibar katika
viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip Airport yatawawezesha wananchi kupata fursa
ya kuchunguza afya zao na kupata elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya
moyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi kutoka Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar wameishukuru Serikali yao kwa kuanzisha maonesho hayo
yanayotoa fursa kwa wananchi wake kupata huduma bobezi za afya bila gharama.
Mariam Suleiman mkazi wa Zanzibar alisema maonesho hayo
yameweza kutoa fursa kwa watoto wake kupimwa moyo bila gharama kwani alikuwa na
wasiwasi kuhusiana na afya za watoto hao.
“Hapa nilipo nimetoka wodini hivi karibuni, watoto wangu hawa
mapacha wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo la kubanwa kifua na daktari alinishauri
nikipata nafasi niwapime moyo, kama bahati leo wamepimwa. Naishukuru sana
Serikali yangu kwa kufanya maonesho haya na kutupa fursa ya kuchunguza afya
bila gharama”, alisema Mariam
Naye Ibrahimu Mohamed mkazi wa Zanzibar alisema Serikali
imeona umuhimu wa wananchi wake kupata huduma za uchunguzi wa afya hivyo
kushirikisha Hospitali za kibingwa ili waweze kuchunguza magonjwa kama ya moyo
ambayo mara nyingi watu hawapimi.
“Tunawashukuru pia wataalamu ambayo mmetumia muda wenu kufika
hapa kwa ajili yetu, tunaomba huu mwanzo mliouanzisha mwaka huu usiishie hapa
bali muendele mara kwa mara kutupa elimu na kutufanyia uchunguzi”, alisema
Ibrahimu
Sambamba na kutoa huduma za elimu na uchunguzi wa magonjwa ya
moyo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika maonesho hayo pia
imeishirikisha na Shirika lisilo la Kiserikali la Heart Team Afrika Foundation
(HTAF) kuihamasisha jamii kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo
wanaotibiwa JKCI.
Comments
Post a Comment