Wafanyakazi wa JKCI watakiwa kufanya kazi kwa kufuata taratibu za utumishi wa umma
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule zawadi kutoka kwa taasisi hiyo mara baada ya kufungua mkutano wa tatu wa baraza jipya la wafanyakazi wa Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi wa wajumbe wa baraza jipya la wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiimba wimbo wa “solidarity forever” wakati wa ufunguzi wa mkutano wa baraza la tatu la wafanyakazi wa Taasisi hiyo.
Baadhi wa wajumbe wa baraza jipya la wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule wakati akifungua mkutano wa baraza la tatu la wafanyakazi wa Taasisi hiyo.
******************************************************************************************************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata taratibu za utumishi wa Umma hii ikiwa ni pamoja na kuwa na weledi na nidhamu ya kazi.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya
ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule wakati akifungua mkutano wa tatu wa baraza jipya
la wafanyakazi wa Taasisi hiyo.
Mhe. Mtambule alisema taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi nzuri
ya kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kwa wagonjwa ndani na nje ya nchi ni
muhimu wafanyakazi hao wakakumbuka kufuata maadili ya kazi zao ili sifa iliyopo
ibaki kama ilivyo.
“Sisi kama viongozi wa Serikali na Wananchi tunajivunia kuwa
na taasisi hii ambayo inatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na kuokoa
maisha ya wagonjwa, hospitali hii ni moja ya vivutio vya utalii tiba vilivyopo
hapa nchini”.
“Ninawapongeza kwa kufungua matawi yenu mengine Oyster bay na
Kawe, kuwepo kwa kliniki hizi kumesaidia watu wengi zaidi kufikiwa na huduma za
kibingwa za matibabu ya moyo kwa haraka
zaidi”, alisema Mhe. Mtambule.
‘Ninampongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
uwekezaji mkubwa alioufanya katika sekta ya afya hii ikiwa ni pamoja na kununua
vifaa tiba vya kisasa na kusomesha wataalamu wabobezi jambo lililosababisha wananchi
wengi kupata huduma za kibingwa za matibabu ndani ya nchi”,
Aidha Mkuu wa Wilaya hiyo alisema wilaya ya Kinondoni itazidi
kushirikiana na taasisi hiyo kwa kufanya kambi maalumu ya matibabu ya moyo ili
wananchi wengi wapate huduma za elimu, uchunguzi na matibabu ya moyo.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge aliwashukuru wafanyakazi wa taasisi hiyo kwa kufanya kazi kwa
ushirikiano na kujitoa na kuwaomba kuendelea kuwa moyo wa huruma kwa wagonjwa
wanaowahudumia.
Dkt. Kisenge
alisema moja ya mafanikio ya kujivunia yaliyopatikana katika taasisi hiyo ni
kuwepo kwa huduma ya kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi
mahali walipo ijulikanayo kwa jina la Tiba Mkopa ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Outreach Services ambapo hadi sasa imeshawafikia wananchi zaidi ya 22,000.
“Baadhi ya
wananchi tuliowaona tuliwakuta na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya
kibingwa na kuwapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu, kuna ambao wametoka
katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi tunashukuru tumeweza kuokoa maisha yao”,
alisema Dk. Kisenge.
Naye Afisa wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Vaileth Ndeza alisema
mabaraza ya wafanyakazi yanaratibiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo na
kutoa pongezi kwa taasisi hiyo kutekeleza matakwa ya sheria kwa kuwa na
mkataba unaounda baraza la wafanyakazi.
“Siku ya leo JKCI imezindua baraza jipya la tatu la wafanyakazi
nimewafundisha wajumbe wapya wa baraza wajibu wao ambao ni kumshauri mwajiri
juu ya hatua za kuongeza tija na ufanisi katika kutoa huduma na kumshauri
mwajiri juu ya mabadiliko ya sheria na kanuni za utumishi”.
“Kumshauri mwajiri juu ya mambo muhimu yanayohusu maslahi ya
wafanyakazi, mazingira ya kazi, upatikanaji wa vitendea kazi, mawasiliano bora
sehemu za kazi posho za wafanyakazi na kupokea, kujadili na kuthibitisha
mipango ya makisio ya mapato na matumizi ya taasisi” alisema Vaileth.
Vaileth
aliwataka viongozi wa baraza hilo kufanya vikao hivyo mara kwa mara kwa
kutekeleza matakwa ya kisheria na kusema kuwa taasisi nyingi zimekuwa zikiunda mabaraza
ya wafanyakazi lakini wameshindwa kufanya mikutano kutokana na changamoto
mbalimbali wanazokutana nazo.
Katibu wa Chama
cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) mkoa wa Dar es Salaam Edward
Mwashitanda alisema ni muhimu wafanyakazi
wa taaasisi hiyo wakawezeshwa maslahi yao kwani wanafanya kazi kwa uweledi na
utaalamu wa hali ya juu wa kuokoa maisha ya wagonjwa.
Mwashitanda
alisema anaamini baraza hilo la wafanyakazi litaleta mabadiliko katika taasisi hiyo
kwa kuendelea kushirikiana kitaalamu katika kutoa huduma nzuri na bora kwa wananchi.
Comments
Post a Comment