Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu, Mary Maganga akimsikiliza daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na
kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elius
Birago alipotembelea banda la taasisi hiyo kuangalia huduma ya uchunguzi
na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa katika maonesho ya Kimataifa ya Wiki
ya Usalama na Afya Mahali Pa kazi yaliyofanyika katika viwanja vya Mandewa mkoani Singida.
Wananchi wa Singida wakisubiri kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa
zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika maonesho
ya Kimataifa ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali Pa kazi yaliyomalizika jana katika viwanja vya Mandewa mkoani Singida.
*******************************************************************************************************************************************************************************************
Na
Jeremiah Ombelo - Singida
Watu 383 wamepata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu
ya upimaji na matibabu iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) mkoani Sungida.
Huduma
hiyo ya upimaji ilitolewa bila malipo katika maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya
Usalama na Afya Mahali Pa kazi yaliyomalizika jana katika viwanja vya Mandewa mkoani Singida.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kambi hiyo daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na
kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elius
Birago alisema walitoa huduma za uchunguzi,
matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa watu wazima 364 na watoto 19.
“Watu
44 wakiwemo watu wazima 42 na watoto wawili tuliwakuta na matizo makubwa ya
moyo yakiwemo ya kuziba kwa mishipa ya damu, umeme wa moyo na valvu, wagonjwa
hawa wanahitaji kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu ya kibingwa tumewapa
rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu”.
“Kwa
upande wa jinsia wanawake walionyesha mwitikio mkubwa zaidi kwani walikuwa 258 na
wanaume 125 hali hii ni kiashiria cha ongezeko la uelewa wa umuhimu wa kupima afya
miongoni mwa wanawake ukilinganisha na wanaume”, alisema Dkt.Birago.
Dkt.
Birago alisema katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za
kibingwa za matibabu ya moyo Taasisi hiyo inatoa huduma ya kuwafuata wananchi
mahali walipo ijulikanayo kwa jina la Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
huduma hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwani watu wengi wamepata nafasi ya
kupima afya za mioyo yao na kupata matibabu bila malipo yoyote yale.
“Ninaishukuru
Serikali ya awamu ya sita kwa kuwasomesha wataalamu wetu na kununua vifaa tiba
vya kisasa na hivyo wananchi wengi zaidi kupata huduma za kibingwa za matibabu
ya moyo. Ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupima afya zao pale
watakaposikia kuna kambi za matibabu ya moyo kwa kufanya hivyo watatambua afya
za mioyo yao na kuanza matibabu mapema kwa wale watakaokutwa na matatizo”, alisema
Dkt. Birago.
Nao
wananchi waliopata nafasi ya kupima afya zao walishukuru kwa huduma waliyoipata
na kusema kuwa imewasaidia kufahamu hali za mioyo yao na kujua jinsi gani
wanaweza kujilinda ili wasipate magonjwa ya moyo.
“Hii
ni mara yangu ya kwanza kupima moyo, nashukuru kwa huduma niliyoipata nimepata
huduma ya kiwango cha juu bila kulipa fedha yoyote ile, nimeelekezwa jinsi ya
kufuata mtindo bora wa maisha unavyoweza kunisaidia nisipate magonjwa yasiyoambukiza
yakiwemo ya moyo”, alishukuru Joseph Chacha mkazi wa Mandewa.
“Mwanangu
akicheza na wenzake anachoka haraka na kutokwa na jasho jingi pia ukuaji wake
ni wa shida, aliwahi kuandikiwa kufanya vipimo vya moyo lakini sikuwa na uwezo
wa kulipia. Baada ya kusikia wataalamu wa moyo wako hapa nikaona nimlete baada
ya kupima amekutwa na shida nimepewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI”.
“Ninawashukuru
wataalamu wa moyo kwa kumtibu mwanangu na kugundua tatizo alilokuwa nalo
ninaamini atatibiwa na atapona,
ninawaomba kinamama wenzangu ambao hawana uwezo wa kifedha wasikate tamaa bali
wawe na ujasiri pindi wakisikia kuna madaktari wako katika maeneo yao wanafanya
kambi za matibabu waende kupata huduma
kama nilivyofanya mimi”, alishukuru Asha Shabani mkazi wa Iramba.
Huduma
zilizokuwa zinatolewa katika maonesho hayo ni za upimaji wa shinikizo la damu, kiwango cha
sukari kwenye damu, kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, kipimo cha mfumo wa
umeme wa moyo, uwiano baina ya urefu na uzito, elimu ya lishe bora, ushauri wa
kiafya kuhusiana na magonjwa ya moyo ikiwemo matumizi sahihi ya dawa na ushauri
wa magonjwa yatokanayo na kazi.
Comments
Post a Comment