Serikali yawashukuru wataalamu wa afya nchini kwa kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa - Dkt. Mollel
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Godwin
Mollel akizungumza na madaktari wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) waliokuwa wakiwaudumia wagonjwa waliolazwa wodini wakati wa ziara yake ya
kikazi katika Taasisi hiyo Jana Jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Godwin Mollel amewashukuru wataalamu wa afya nchini kwa moyo wao wa
uzalendo wa kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa.
Mhe. Mollel ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi
wa Taasisi ya Moyo Jakaja Kikwete (JKCI) aliowakuta wanawatibu wagonjwa wodini
na kliniki wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya leo katika Taasisi hiyo
iliyopo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mollel alisema katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na
changamoto nyingi za maradhi wataalamu hao wa afya wamekuwa mkono wa Serikali
kwa kuhakikisha wananchi wanakuwa salama kwa kutoa huduma bora za afya bila ya
kuchoka.
“Kuna wakati mnafanya kazi katika mazingira magumu bila ya kuwa
na hofu yoyote ile jambo la muhimu ni kuchukuwa tahadhari za msingi”, alisema
Dkt. Mollel.
Alisema katika Hospitali nyingi alizotembelea asilimia 78 ya
matatizo yaliyopo ni kutokana na viongozi wa maeneo husika kutokufanya kazi
vizuri au kutokujua majukumu yao ya kazi na hivyo kuwakatisha tamaa watumishi
wengine ambao pamoja na mazingira hayo magumu waliweza kufanya kazi zao kwa
weledi.
Dkt. Mollel alipongeza , “Hapa JKCI ninawapongeza kwa juhudi
zenu za kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wagonjwa mnaowatibu. Katika maeneo
mengine siyo kama dawa hakuna bali kuna udokozi pia wanatenga fedha kidogo za
kununulia dawa ukilinganisha na bajeti husika”,.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof.
Mohamed Janabi alisema kwa mwaka 2020 walitumia kiasi cha shilingi
milioni 158 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kuwasomesha wafanyakazi
20 wa kada mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Mwaka 2020 wafanyakazi 11 waliokuwa masomoni ndani na nje
ya nchi walimaliza masomo yao na kurudi kazini na kwa mwaka wa fedha 2020/21
wafanyakazi 13wameanza masomo”, alisema Prof.Janabi.
Prof. Janabi alisema
Taasisi kwa kuwasomesha wafanyakazi hao imeweza kuzalisha wataalamu wa fani
mbalimbali ambao baada ya kumaliza masomo yao wameweza kuongeza idadi ya
mabingwa na hivyo kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Comments
Post a Comment