TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE YAWATAKA WAAJIRIWA WAPYA KUWAJIBIKA, KUCHAPA KAZI
WAAJIRIWA wapya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), wametakiwa
kuwajibika na kuchapa kazi kwa bidii ili kuendeleza juhudi za kuokoa maisha ya
watu wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo wanaofika kupata matibabu katika taasisi
hiyo.
Rai hiyo
imetolewa mapema leo na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi
alipokuwa akizungumza na waajiriwa wapya saba walioajiriwa na Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kupangiwa kutoa
huduma katika Taasisi hiyo.
“Taasisi
hii imepata mafanikio makubwa tangu ilipoanzishwa hadi sasa, baadhi yenu
mmekuwa sehemu ya juhudi hizi, kwa sababu kwa nyakati mbalimbali mmewahi
kujitolea kufanya mafunzo kwa vitendo hapa”.
“Kwa
juhudi zile zile endeleeni kuchapa kazi, kila mmoja awajibike katika nafasi
yake, mtaona faida ya kazi na juhudi zenu, hakikisheni mnawahi kazini, binafsi
huwa sitaki kusikia habari za foleni, mvua kwamba ni sehemu ya sababu ya
kuchelewa kufika kazini,” amesisitiza.
Ameongeza
“Tuna mafanikio makubwa, tangu kuanzishwa kwa Taasisi hii, miaka minne ya
utendaji kazi wetu vifo vilivyotokea katika chumba cha upasuaji mdogo wa bila
kufungua kifua kupitia tundu dogo kwenye paja ni asilimia 1.5 yaani sawa na
wagonjwa wanane tu waliopoteza maisha katika kipindi chote hicho.
“Tumeweza
kupandikiza vifaa visaidizi vinavyousaidia moyo kufanya kazi vizuri (Pacemaker) kwa wagonjwa 56, CRTD kwa wagonjwa wagonjwa 11,
tumevuna na kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (Coronary Artery Bypass Graft - CABG) wagonjwa
82 na tumezibua valvu zilizokuwa zimeziba bila kufanya upasuaji wa kufungua
kifua kwa zaidi ya wagonjwa 1,000 hadi sasa,” amebainisha.
Amewataka
waajiriwa hao kutosita kuuliza wale waliowatangulia kazini mahala popote
watakapokutana na changamoto mbalimbali ili kuweza kuzitatua na kuzingatia
uvaaji nadhifu wa mavazi yenye staha.
Akizungumza
kwa niaba ya waajiriwa wapya wenzake, Daktari Winnie Masakuya amesema wapo
tayari kufanya kazi kwa juhudi na maarifa waliyojaliwa na Mwenyezi Mungu katika
kuwahudumia wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
“Hatutaiangusha
Taasisi yetu,” amemhakikishia Prof, Janabi katika kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa
na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Fedha
wa JKCI, Agnes Kuhenga.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi
akizungumza na waajiriwa wapya saba walioajiriwa na Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kupangiwa kutoa
huduma katika Taasisi hiyo iliyopo
Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na waajiriwa wapya saba walioajiriwa na Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kupangiwa kazi
katika Taasisi hiyo mara baada ya
kumaliza mafunzo ya siku tatu kwa
waajiriwa hao leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na
Fedha wa JKCI Agnes Kuhenga.
Comments
Post a Comment