Wakazi wa Temeke wachangamkia huduma za uchunguzi, matibabu ya moyo iliyotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Jukwaa la One Stop Jawabu

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi  akimpima shinikizo la damu (BP) mwananchi  aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya  uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika viwanja vya MwembeYanga wilayani Temeke kupitia jukwaa la One Stop Jawabu  ambapo JKCI ilitoa bila malipo huduma za upimaji,  matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa watu 150.


SEPTEMBA 24, 2020 – DAR ES SALAAM

Mwitiko wa wakazi wa Wilaya ya Temeke, jijini hapa kwenda kufanyiwa uchunguzi na matibabu dhidi ya magonjwa ya moyo katika viwanja vya mwembe yanga, umekuwa mkubwa. 

Wananchi hao wamepata fursa hiyo ya kuchunguzwa na kutibiwa bila malipo pamoja na kupewa ushauri wa lishe jinsi gani wanaweza kuendelea kutunza afya ya moyo na mwili kwa ujumla ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza katika Viwanja vya Mwembe Yanga, Wilayani humo, katika Jukwaa hilo lililoratibiwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi alisema ni muhimu wananchi kuzingatia mfumo bora wa maisha ili kujilinda dhidi ya magonjwa hayo ambayo kasi yake inazidi kuongezeka duniani.

“Kadri uchumi wa nchi unavyokua, kasi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo ya moyo, kisukari, kuharusi, saratani na mengineyo yaliyomo kwenye kundi hilo nayo itaongezeka zaidi endapo jamii haitachukua tahadhari kuyaepuka, ili kuyaepuka magonjwa haya jamii izingatie pia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, kuepuka unywaji pombe, uvutaji wa sigara na kuzingatia uchunguzi wa afya mara kwa mara," alisema.

Aliongeza “Naomba mni-quote (mninukuu vizuri), Magonjwa ya moyo, kisukari, saratani... yataongezeka zaidi kwa sababu, kadri uchumi wa nchi zetu unakwenda juu na haya magonjwa yatakwenda juu, ikiwa hatutachukua tahadhari.

“Kwa sababu, watu sasa hivi wana uwezo wa kununua chakula kingi zaidi, bahati mbaya chakula kipi? Hilo ni suala jingine kabisa, watu wengi sasa hivi hata kama hawana usafiri binafsi, zipo bodaboda, daladala wanazitumia kwa hiyo yale mazoezi yamepungua sana.

“Maisha yetu yamekuwa marefu zaidi (umri wa kuishi umeongezekai), kwa sababu unapokuwa na hospitali, vituo vya afya, unapofanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, wagonjwa wanaibuliwa mapema, wanatumia dawa kwa wakati, mimi si Mungu, nazungumza kama daktari, kwa hatua hiyo unaongeza maisha yake,” alibainisha.

Aliongeza “Sasa kadri umri wetu unavyokuwa mkubwa ndivyo yale magonjwa ya watu wazima tunakutana nayo, hili la mazoezi…huwa natoa mfano mara nyingi, mimi nilikuwa nakaa kinondoni, nasoma Hannanasif, nilikuwa asubuhi nachungulia ule mkondo kama maji hayapo, unakatiza pale unakwenda shule.

“Lakini sasa hivi watoto wangu hawatembei, asubuhi ‘school bus’, itamchukua, bodaboda au bajaji, mazoezi yamepungua sana, kuna suala la elimu, kwa sababu kama mgonjwa wa ‘presha’ anakunywa dawa wiki moja na kufikiri kwamba amepona, sisi upande wetu wa sekta ya afya tunapaswa kuongeza nguvu ya elimu, tusiongeze nguvu zaidi kwenye tiba pekee, tiba na kinga zinapaswa kwenda pamoja,” alisisitiza.

Aliongeza “Kwa hiyo haya magonjwa yataongezeka na ni bahati mbaya kwamba ni magonjwa ya nchi zilizoendelea na sisi tumo kwenye kundi hili, ni kujua tu jinsi gani sasa tutafanya elimu ya kinga zaidi, kama jinsi Dc. Gondwe alivyochukua hatua.

“Itafika mahala watu watatambua kwamba kabla hata hajaambiwa, ni muhimu kwake kwenda kuchunguza afya, tukipata kundi kubwa la wananchi wanaokwenda wenyewe kuchunguzwa afya bila kusubiri kuambiwa, tutakuwa tumeokoa jamii.

“Kusema ukweli, Watanzania wengi hawana utamaduni wa kupima afya, ni gharama kidogo... zinapotokea huduma kama hizi (One Stop Jawabu) hapo ndiyo mara nyingi tunapata wagonjwa wengi kuliko kawaida, kwa sababu wengi huja tu kwa lengo la ‘ku-check’ Afya zao.

“Kuna mtu, hatuwezi kutaja jina... Nimempima nimekuta tayari moyo wake umeshakua mkubwa... Bahati mbaya magonjwa ya moyo hayaoneshi dalili hadi hali inapokuwa mbaya ... Tumempa rufaa kuja kule JKCI,” alibainisha.

Aliongeza “Katika viwanja hivi, tumetoa elimu ya lishe na dawa kwa wale tuliowakuta  na matatizo, tumetoa huduma hizi bila malipo, tunashukuru kwa fursa hii, tumeibua wagonjwa wapya yupo hadi mwenye presha 200 kwa 100, mama mmoja alikuwa hadi anatetemeka, tumempa dawa.

“Wananchi tunawaomba wakate bima ya afya ili kusaidia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu dhidi ya magonjwa haya, tukikata wengi, Serikali itasaidia wale wachache ambao watashindwa kutokana na uwezo walionao nah ii itakuwa imesaidia kufikia lengo la ‘Universal Health Coverage’ (afya kwa wote),” alisisitiza.

Akizungumza, Dc. Gondwe ameipongeza JKCI kwa kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge kwenda kuhudumia wananchi katika Wilaya hiyo ya Temeke.

“Alikuwa wa kwanza kukubali kutoa huduma katika One Stop Jawabu, wameweza kugundua na kuwapa dawa bila malipo wananchi, tumefurahi, waliogundulika na matatizo yanayohitaji uchunguzi zaidi wamepewa rufaa kwenda kule JKCI, hii ni fursa hadimu kupatikana.

“Ametudokeza yupo tayari pia kufanya mobile clinic, kwenda kwenye vituo vyetu vya afya na hospitali za mkoa wa Dar es Salaam, hili tunakwenda kulijadili baada ya kufanya tathmini ya jukwaa hili la One Stop Jawabu, tutalieleza vizuri,” alibainisha.

Aliongeza “Hili la bima ya afya ni zuri na lipo, uzuri Tanzania kila mwananchi anaweza kujipimia kwa CHF na NHIF na zipo pia taasisi binafsi zinazotoa huduma za bima ya afya, ukiwa na bima ya afya inakuwa rahisi kupata huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo na mengine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Godwin Gondwe aliyefika katika   banda la Taasisi hiyo jana katika viwanja vya MwembeYanga kupitia jukwaa la One Stop Jawabu  kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo zilizokuwa zinatolewa na Taasisi hiyo. JKCI  ilitoa bila malipo huduma za upimaji,  matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa watu 150.

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari